Waalimu nchini Kenya hatimaye wamesimamisha mgomo wao na wanafunzi katika shule za umma watarudi madarasani Jumatatu, Oktoba 5, 2015.
Umoja wa vyama vya waalimu Kenya (Kuppet) ulitangaza uamuzi huo Jumamosi. Vyama hivyo vilifanya mikutano tofauti na kamati zao za uamuzi kabla ya kuwatangazia wanachama wao warudi madarasani Jumatatu.
Vyama hivyo pia vilitaka tume ya huduma za waalimu (TSC) kulipa waalimu mishahara ya mwezi Septemba.
Katibu Mkuu wa chama cha KNUT, Wilson Sossion alisema hata hivyo, chama hicho hakitajitoa katika kesi ambayo TSC walikata rufaa kupinga uamuzi wa kuwapa waalimu nyongeza ya asilimia 50 hadi 60 ya mishahara yao.
"Waalimu watarudi katika mgomo baada ya siku 90 endapo TSC haitatekeleza amri ya mahakama," alisema Bw. Sossion.
Siku ya Alhamisi mahakama Kenya iliamuru waalimu kurejea mashuleni mara moja.
Waalimu wa Kenya wamekuwa katika mgomo kwa zaidi ya mwezi mmoja wakidai serikali ilipe nyongeza ya mishahara kwa asilimia 50 kama ilivyoamuliwa na mahakama hapo awali. Serikali ya Rais Uhuru Kenyatta imesema haina uwezo wa kuongeza mishahara kwa kiwango hicho.