Hafla hiyo ilifanyika kwenye ofisi za wizara ya mambo ya nje ya Marekani mjini Washington DC.
Waziri wa mambo ya nje wa Kenya, Monica Juma, ambaye aliongoza ujumbe wa Kenya, alitia saini makubaliano hayo, ambayo pia yananuia kuimarisha hali ya usalama katika eneo la Afrika Mashariki na kati, ambapo Marekani iliwakilishwa na naibu wa waziri wa mambo ya nje, John Sullivan.
"Rais Uhuru Kenyatta alituagiza tushirikiane kwa karibu na kuhakikisha kwamba maeneo yetu ya pembe ya Afrika, Afrika Mashariki na Kati, yako salama kwa uwekezaji… Kwamba yako imara kisiasa, yako huru kidemokrasia na pia kuhakikisha kwamba tuko huru kutokana na tishio kubwa la itikadi kali na ugaidi wa kimataifa," alisema Bi Juma.
"Hii ni kwa sababu hata tukiimarisha mazingira ya uwekezaji bila kukabilina na tishio la ugaidi, bado tutakuwa kwenye hatari," aliongeza.
Wakati wa hafla hiyo, naibu wa waziri wa mambo ya nje wa Marekani, John Sullivan, alisema ziara ya ujumbe huo wa Kenya nchini Marekani, pia inanuia kutamatisha makubaliano kuhusu nafasi ya Marekani katika kuimarisha miundo msingi, usalama wa raia na kusaidia katika masuala ya uongozi bora nchini Kenya.
Baadhi ya maafisa waliokuwemo ni naibu wa waziri wa mambo ya nje anayeshughulika na masuala ya Afrika Tibor Naggy ambaye alisema kuwa hii ni awamu ya kwanza ya mazungumzo yatakayoendelea kwa kipindi kirefu.
"Mpango huu unajumuisha sehemu nne muhimu, za mahusiano kati ya nchi zetu mbili, na unatokana na mkutano kati ya marais wetu wawili mwezi Agosti mwaka jana. Huu ni mkutano wetu wa kwanza na tutaendelea mwaka baada ya mwaka, kuimarisha ushirikiano wetu na kufikia kiwango kipya," alisema Nagy.
Bi Juma aliandamana na maafisa kadhaa waandamizi katika serikali ya Kenya, wakiwemo Waziri wa Usalama wa ndani, Fred Matiang'i na balozi wa Kenya nchini Marekani, Robinson Njeru Githae.
Maafisa hao walitarajiwa kufanya kikao na waandishi wa habari baadaye Jumatano jioni, saa za Washington DC.