Kenya yaongeza medali katika riadha Rio 2016

Conseslus Kipruto, Men's 3000m Steeplechase Final

Kenya imeongeza medali mbili Jumatano - dhahabu na shaba - katika michezo ya Olimpiki 2016 huko Rio de Janeiro katika mita 3000 kuvuka viunzi baada ya Conseslus Kipruto kushika nafasi ya kwanza na medali ya dhahabu akitumia muda wa dakika 8, na sekunde 03.28.

Mkenya mwingine Ezekiel Kemboi alichukua medali ya shaba katika nafasi ya tatu katika muda wa dakika 8, sekunde 08.47. Medali ya fedha ilikwenda kwa Evan Jager wa Marekani ambaye alimaliza katika muda wa dakika 8, sekunde 04.28.

Conseslus Kipruto akiruka kihunzi katika mita 3000

Brimin Kipruto wa Kenya alimaliza katika nafasi ya saba ingawa alikuwa katika kundi ambalo liliongoza kwa muda mrefu katika fainali hiyo.

Sasa Kenya ina jumla ya medali nne za dhahabu, pamoja na tatu za fedha na moja ya shaba na kuwa nchi inayoongoza kwa bara la Afrika kwa kuwa na jumla ya medali nane.

Inafuatiwa na Afrika Kusini ambayo ina jumla ya medali sita.