Kenya: Hatujashindwa kulipa deni la China, habari zinazoenea ni za uongo

Gari dogo likipinda chini ya daraja huku gari moshi likipita kwenye reli ya mwendo wa wastani SGR, Athi River, Kenya. June 3, 2022

Serikali ya Kenya imekanusha ripoti za vyombo vya habari kwamba benki za china zimeitoza faini nchi hiyo ya kiasi cha dola milioni 11 kwa kushindwa kulipwa mikopo yao ambayo waliitumia kufadhili mradi mkubwa wa ujenzi wa reli ya mwendo wa wastan SGR.

Wizara ya Fedha ya Kenya inasema kuwa nchi hiyo haijawahi kushindwa kuwalipa wadai wake. Theluthi moja ya mikopo ya nchi hiyo ni kutoka China.

Baada ya miaka kadhaa ya kukopa fedha kutoka China kufadhili miradi na program za serikali, maswali yanaulizwa kuhusu kama Kenya inaweza kulipa madeni yake.

Alhamisi, katika taarifa yake, Waziri wa Fedha, Ukur Yatani alisema nchi haijawahi kushindwa kuwalipa wadai wake.

Waziri alikuwa akijibu ripoti ya vyombo vya habari kwamba benki za China zimeitoza Kenya faini ya dola milioni 11 kwa kushindwa kulipa mikopo yake iliyochukua kwa ajili ya ujenzi wa reli maarufu kama Standard Gauge Railway.

Gharama ya Ujenzi wa SGR

Rais mstaafu wa Kenya Uhuru Kenyatta (kwa wa kwanza kushoto) akifanya mazungumzo na waziri mkuu wa China Li Keqiang (wa kwanza kulia) mjini Beijing, China. Aug 20 2013


Taifa hilo la Afrika Mashariki lilikopa dola bilioni 4 kujenga reli kutoka bandari ya Mombasa hadi mjini Naivasha, kiasi cha kilometa 100 kutoka mji mkuu.

Seneta Samson Cherargei, mwanachama wa chama tawala cha United Democratic Alliance, ameiambia VOA kuwa serikali iko katika hali nzuri ya kulipa deni lake la shilingi trilioni 10 za Kenya, sawa na dola bilioni 82 za kimarekani.

“Nina imani kuwa deni la shilingi trilioni 10 ambalo Jamhuri ya Kenya inakabiliana nalo bado ni endelevu na serikali inaweza kulilipa na kama bunge, tumehakikisha kwamba tunapokea kila baada ya kipindi fulani katika misingi ya malipo yanayofanywa na serikali kwa deni la umma. Kwahiyo, nina imani kubwa sana kwamba serikali ina uwezo wa kulipa deni lake la umma,” amesema Cherargei.

Mnamo mwezi Juni, bunge lililopita liliongeza kiwango cha deni la umma kufikia dola bilioni 83 ili kuisaidia serikali inayoingia madaraka kuwa na uwezo wa kuisaidia kuendesha program zake.

Sameul Nyandemo anafundisha uchumi katika Chuo Kikuu cha Nairobi. Anasema “Kenya haiwezi kujihimili yenyewe bila ya kukopa lakini lazima watumie fedha vizuri ambazo wanakopa ndani na nje ya nchi.”

Nyandemo anasema “sidhani Kenya imefikia sehemu ambayo inaweza kujimudu yenyewe. Njia bora ambayo tunaweza kufanya ni kupunguza kiwango cha kukopa, kopa pale ambapo ni muhimu na kila unachokopa, watakitumia vizuri.”

Serikali ya Kenya imekopa ‘sana’

Bunge la Kenya likiwa katika kikao, Nairobi, June 10, 2021.

Serikali ya Kenya imelaumiwa kwa kukopa sana katika siku zilizopita na kuweka gharama kubwa kwa miradi yake mikubwa, na kuiacha nchi ikiwa na madeni makubwa ambayo kulipa nayo ina changamoto zake.

Rais mpya Dr. William Ruto anasisitiza kwamba utawala wake utapunguza kukopa fedha kutoka nje na kubuni njia mbadala kwa serikali kufadhili miradi yake.

Nyandemo anasema maafisa wa Kenya watahitaji kuzungumza na China na kukubaliana njia ya jinsi ya kuzilipa fedha hizo katika miaka ijayo.
“Mikopo hiyo ni mikubwa sana. Jaribio la kwanza serikali mpya itakachofanya ama itakuwa kufanya mashauriano tena kwa ajili ya hii mikopo kwa misingi mipya ambayo itakuwa vigumu sana na mingi ya mikopo hiyo ni ya kibiashara na mikopo ya kibiashara siku zote ni ya gharama kubwa. Nadhani njia bora kwa serikali mpya kufanya ni kwenda kwenye mikopo yenye masharti nafuu na kupunguza kiwango ambacho wanakopa, na kutiumia vyema na kupunguza matumizi ya umma,” anasema Nyandemo.

Ruto ameamuru serikali kupunguza matumizi ya pesa

Rais wa Kenya Dr. William Ruto akihutubia waandishi wa habari Sept. 5, 2022


Mwezi uliopita, rais William Ruto aliamuru Wizara ya Fedha kupunguza matumizi ya pesa za serikali kwa kiasi cha dola bilioni 2.5

Sabina Chege ni mwanachama wa upinzani katika bunge, anasema serikali, kupitia shirika la reli nchini Kenya, Kenya Revenue Authority (KRA), inatakiwa kupata fedha kupitia kodi na kupambana na rushwa.

Chege anasema “serikali ya kenya imesisitiza kuhusu ulipaji kodi na kulikuwa na suala jingine la pili la kupambana na rushwa, kwahiyo kulikuwa na mipango madhubuti ya kupata fedha serikali. Tunachokiona hivi sasa na serikali hii iliyopo mamlakani ni kwamba watu ambao wako upande wa utawala wa sasa, hata kesi za rusha, zinaondolewa. Maafisa wa KRA hivisasa wanakhofia kumfuatilia mtu yeyote kwaababu hawajui kama watamgusa mtu ambaye si sahihi. Lakini utendaji umekuwa ukishuka,”

Serikali ya Kenya imetoa changamoto kwa mamlaka ya kitaifa ya kukusanya kodi KRA kukusanya kiasi cha dola bilioni 25 ifikapo mwisho wa mwaka huu, ambazo zitasaidia katika program za maendeleo.