Mahakama kuu kenya yatoa tamko kuhusu uchaguzi ujao

Jengo la mahakama mjini Nairobi, Kenya

Baadhi ya wabunge nchini Kenya wanamisimamo tofauti juu ya mabadiliko ya mara kwa mara kuhusu uchaguzi nchini humo

Mahakama kuu nchini Kenya imesema uchaguzi mkuu lazima ufanyike kabla ya kumalizika mwezi Machi 2013, vinginevyo uchaguzi unaweza kufanyika mapema kabla ya hapo kama serikali ya kushirikiana madaraka nchini humo itavunjwa.

Tarehe ya uchaguzi imezusha mjadala mkali nchini Kenya. Katiba mpya nchini Kenya iliyopitishwa mwaka 2010, ilitaka uchaguzi mkuu ujao ufanyike Agosti 14 mwaka huu. Lakini baadhi ya wabunge wameshinikiza kusogezwa kwa uchaguzi hadi mwezi Disemba kwa sababu za maandalizi.

Mahakama iliamua Ijumaa kwamba uchaguzi unatakiwa ufanyike ndani ya kipindi cha siku 60, mwisho wa mhula wa bunge wa miaka mitano, ambao unafikia Januari 15, mwaka 2013.

Mahakama imeacha wazi uwezekano wa kuwepo tarehe za mapema, kama Rais Mwai Kibaki na Waziri Mkuu, Raila Odinga wanakubali kulivunja bunge kabla ya wakati huo.

Uchaguzi huo, utakapofanyika, utakuwa uchaguzi wa kwanza nchini humo tangu uchaguzi wa mwaka 2007 uliogubikwa na kasoro katika matokeo ya kura. Ghasia za mashambulizi ya kikabila baada ya uchaguzi huo ziliuwa kiasi cha watu 1,300.

Mahakama ya kimataifa ya uhalifu-ICC hivi sasa inawachunguza viongozi sita maarufu nchini Kenya walioshutumiwa kwa kupanga ghasia za baada ya uchaguzi.

Serikali ya ushirikiano madaraka Kenya imekuwa pamoja tangu mwaka 2008 licha ya mivutano kati ya Rais Kibaki na Waziri Mkuu Odinga, ambao walikuwa wapinzani katika uchaguzi wa mwaka 2007.