Polisi huko kaskazini mwa Kenya wanasema mlipuko unaodhaniwa kuwa bomu la kutegwa ardhini umemuuwa afisa mmoja wa polisi na kuwajeruhi wawili wengine kwenye kambi moja ya wakimbizi ya Dadaab.
Maafisa wa polisi wanasema mlipuko wa Jumatatu ulitokea wakati maafisa wa polisi walipokuwa wanasafiri kwa kutumia gari.
Hili ni tukio la karibuni katika mifululizo ya mashambulizi madogo madogo ambayo imeikumba nchi ya Kenya tangu serikali yake ilipopeleka wanajeshi kuingia katika nchi ya Somalia kupambana na wanamgambo wa kundi la al-Shabab. Kenya inawashutumu wapiganaji wenye uhusiano na al-Qaida kwa kuwateka nyara watalii wa kigeni kwenye ardhi ya Kenya.
Wanamgambo hao wanasema wanapigana kuiangusha serikali ya Somalia inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa na kuweka mfumo mkali wa sheria wa ki-Islam.
Dadaab ni makazi ya zaidi ya wakimbizi 400,000 kutoka nchini Somalia.
Polisi mmoja ameuwawa na wengine kujeruhiwa kufuatia mlipuko kwenye kambi ya wakimbizi ya Dadaab