Kenya: Bei ya mafuta yapanda baada ya serikali mpya kuondoa ruzuku

Rais mpya wa Kenya William Ruto akila kiapo, Septemba 13, 2022.

Bei ya mafuta nchini Kenya imepanda kwa kiwango cha juu Alhamisi baada ya serikali mpya kuondoa ruzuku na kuzidisha hali ngumu ya maisha kwa wanainchi ambao tayari wanakabiliwa na matatizo makubwa ya kiuchumi.

Bei ya petroli imeongezeka kwa shilingi 20 na kufikia shilingi 179.20 kwa lita, huku bei ya dizeli ikipanda kwa shilingi 20 nayo bei ya mafuta ya taa ikiongezeka kwa shilingi 25, mamlaka ya nishati na mafuta ya petroli (EPRA) imesema.

Bei hiyo mpya ambayo itaendelea kutekelezwa hadi Oktoba 14 imetangazwa muda mfupi baada ya rais mpya wa Kenya William Ruto kuingia madarakani Jumanne, akiapa kuondoa ruzuku ya chakula na mafuta.

Kenya inakabiliwa na hali ngumu ya uchumi kutokana na kupanda kwa bei ya mafuta ghafi duniani na mwaka jana ilichukua hatua za kuwapeusha wanunuzi na athari za bei ya juu ya rejareja.

Kenya ilitumia shilingi bilioni 144, karibu asilimia 86 ya mapato ya utali mwaka huu ili kugharimia ruzuku ya mafuta, kulingana na takwimu za serikali.