Kenya Airways kuzindua safari za moja kwa moja kwenda Marekani

Ndege za Shirika la Ndege la Kenya

Shirika la ndege la Kenya Airways Alhamisi limeanza kuuza tiketi kwa ajili ya uzinduzi wa safari zake kati ya Nairobi na New York. Shirika hilo linapanga kufanya safari ya kwanza Oktoba 28, 2018.

Wakenya na wasafiri wengine wataweza kununua tiketi zao mapema kwa bei ya Dola za Kimarekani 869, na kuwa tiketi hizo kwa bei hiyo poa ni chache na bei zitaongezeka kadiri watu watavyoendelea kufanya manunuzi.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa KQ Michael Joseph uzinduzi huo ni hatua muhimu kwa shirika hilo ambayo imefatia mipango mipya ya kifedha iliyotekelezwa na shirika hilo, akiongeza kuwa safari hiyo italiwezesha shirika hilo kuimarika na kuendelea kuingiza faida.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kenya Airways Sebastian Mikosz amesema safari hizo zitakuwa na manufaa makubwa kwa shirika hilo na kuimarisha ukuaji wa biashara yake.

"Huu ni wakati wa kusisimua sana kwetu. Mpango huu unawiana vyema na mpango wetu wa kuvutia abiria kutoka kwa mashirika na kampuni mbalimbali pamoja na watalii wa daraja la juu ambao wanapendelea kutembelea Kenya na Afrika," amesema.