Mkuu wa mataifa ya kupambana na ukimwi katika Umoja wa Mataifa amemtaja mwanamitindo maarufu wa Marekani, Kenneth Cole kuwa balozi wa kimataifa wa hisani.
Mkuu wa UNAIDS, Michel Sidibe siku ya Jumanne alisema Cole ambaye ana historia ya muda mrefu katika harakati za ukimwi anaweza kuwa na “mchango wa dhahiri na wenye nguvu” kuelekea katika kufanikisha lengo la kimataifa la kumalizwa ukimwi ifikapo mwaka 2030. Sidibe amempongeza Cole kwa “nia ya dhati, huruma na utatuzi,” na kusema Cole atasaidia kuhakikisha kwamba “hakuna anayeachwa nyuma.”
Cole ambaye amejipatia umaarufu mkubwa katika kubuni nguo na viatu vya gharama ni mmoja wa wanamitindo wa kwanza kuzungumza hadharani kuhusu HIV jambo ambalo limeipiga nguvu sana sekta ya mitindo katika miaka ya 1980. Cole aliandaa kundi la watu mashuhuri wakiwemo wana mitindo Christie Brinkley na Beverly Johnson na mpiga picha maarufu Annie Leibovitz kutengeneza matangazo ya umma wakitaka utafiti zaidi ufanywe kuhusu ukimwi.
Wakati huo ukimwi ulibeba unyanyapaa mkubwa kwahiyo kujihusisha na majina na nyuso maarufu ilikuwa ndiyo njia ya kupata uungaji mkono katika suala hilo.
Cole alifanya kazi na taasisi ya utafiti wa ukimwi inayojulikana kama amfAR tangu mwaka 1987, akijiunga kama mjumbe wa kwanza na baadaye kutumika kama mwenyekiti. Cole alisema kwamba ana matumaini ya kuchanganya kazi yake ya taasisi mbili. Alisema “ukimwi unaweza kumalizwa kama mzozo wa afya ya umma kama rasilimali zitakuwepo.”