Katiba-Russia hairuhusu Putin kugombea muhula wa tano

Rais Vladimir Putin

Vladimir Putin, ambaye ametumikia nafasi ya urais na waziri mkuu wa Russia tangia 1999, ameapishwa tena kwa muhula wa nne kama rais Jumatatu katika sherehe zilzofanyika Ikulu ya Kremlin.

Akiweka mkono wake juu ya nakala ya katiba iliyorembwa kwa dhahabu, Putin ameapa kuwatumikia wananachi wa Russia, akilinda maslahi ya haki na uhuru wao, na kutetea uhuru wa Russia na baada ya hapo kutoa hotuba ya kuchukua madaraka.

“Ninaona hili kama ni jukumu langu na dhamiri ya uhai wangu wote kufanya kila kitu kwa ajili ya Russia, kwa wakati uliopo na siku za usoni, amani na mafanikio yake, kwa ajili ya kuijali na kuendeleza taifa letu bora, kwa maslahi ya kila familia ya Warusi," amesema Putin.

Putin hatoweza kugombea nafasi hiyo kwa muhula wa tano kama rais. Ataweza kufanya hivyo iwapo kutakuwa na mabadiliko ya katiba ambayo inakataza kugombea urais mihula zaidi ya miwili mfululizo.

Kuapishwa kwa Putin kwenye Ikulu ya Kremlin kumekuja siku mbili baada ya maandamano yaliyofanyika nchi nzima kupinga kuanza kwa muhula mwengine wa miaka sita ya urais wa kiongozi huyo wa zamani wa shirika la ujasusi la Russia-KGB.

Siku ya Jumamosi, kiongozi maarufu wa upinzani nchini Russia, Alexei Navalny, amekamatwa mara baada ya kuwasili katika maandamano katikati ya mji wa Moscow. Navalny na mamia ya wafuasi wake walishikiliwa na polisi wakati wa maandamano hayo Moscow na miji mingine 90. Navanly aliachiwa Jumapili.

Putin aliivamia Crimea iliyoko Ukraine wakati wa kipindi cha utawala wake wa karibuni na pia alishirikiana na kiongozi wa Syria Bashar al-Assad katika kampeni ya kijeshi huko Syria.