Kasisi wa kanisa la Katoliki auwawa na moto Nigeria

Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari

Watu wenye silaha wamemchoma moto hadi kufa kasisi wa kanisa la Katoliki na kumjeruhi mwenzake kaskazini mwa Nigeria Jumapili.

Polisi wanasema hili ni tukio la karibuni kabisa kutokea likizusha wasiwasi wa usalama kabla ya uchaguzi mkuu mwezi ujao.

Nigeria itapiga kura kwa ajili ya rais mpya Februari 25 lakini utekaji kwa ajili ya kupata malipo ya fidia na mauaji yanayofanywa na magenge ya uhalifu yenye silaha upande wa kaskazini yamesababisha hofu kwamba uchaguzi unaweza usifanyike katika baadhi ya maeneo.

Wasio Aboodum , msemaji wa polisi katika jimbo la Niger alisema katika taarifa kwamba watu wenye silaha walichoma moto makazi ya kasisis Isaac Achi wa kanisa la Saints Peter katika eneo la Paikoro baada ya kushindwa kuingia ndani majira ya saa tisa usiku kwa saa za Nigeria.

Kasisi huyo aliungua moto hadi kufa wakati mwenzake aliyejulikana kwa jina la Collins aliyekuwemo ndani alipigwa risasi na kujeruhiwa wakati akijaribu kutoroka. Anatibiwa katika hospitali moja ya ndani.

Gavana wa jimbo la Niger Sani Bello amesema huu ni wakati wa masikitiko kwa kasisi kuuwawa kwa njia hiyo .

Amesema magaidi hao wamepoteza mwelekeo na hatua madhubuti zinastahili kuchukuliwa ili kumaliza kabisa vitendo hivyo vya uhalifu na mauaji.