Kampuni ya usafirishaji ya Denmark, Maersk, na ile pinzani ya Ujerumani ya Hapag-Llyoyd, Jumanne zimesema meli zao za makontena zitaendelea kuikwepa njia ya bahari ya sham ambayo inazifikisha mpaka mfereji wa Suez, kufuatia shambulizi la mwishoni mwa juma kwa moja ya meli za Maersks.
Makampuni hayo makubwa yatabadilisha njia ya safari zake kupitia kusini mwa Afrika kwa sababu wanamgambo wa kihouthi wa Yemen kushambulia meli katika bahari ya Sham.
Hatua hiyo inatishia kudhoofisha usafirishaji na kuongeza bei ya bidhaa, kuleta hofu ya kuchochea mfumuko mpya wa bei duniani.
Kampuni zote hizo kubwa za usafirishaji zilisimamisha safari zote katika bahari hiyo kwa saa 48 kufuatia majaribio ya wanamgambo wa Kihouthi kupanda meli ya Maersk Hangzhou.
Helikopta za jeshi la Marekani zilikabiliana na shambulizi hilo na kuwauwa wanamgambo 10.