Kampeni ya Trump yasisitiza "watu wengi mno" walihudhuria mkutano Tulsa

Rais Donald Trump wa Marekani akihutubia mkutano wa kisiasa mjini Tulsa, Oklahoma, Jumamosi Juni 20, 2020. (Picha ya AP/Sue Ogrocki)

Timu ya kampeni ya rais wa Marekani Donald Trump Jumapili ilipuuza madai kuwa watu hawakujitokeza kwa wingi kwenye mkutano wa kisiasa uliofanyikia Jumamosi usiku kwenye ukumbi wa BOK mjini Tulsa, Oklahoma, “kutokana na tishio la maambukizi ya virusi vya corona au uwezekano wa kutokea kwa maandamano.”

Ukumbi huo wenye uwezo wa kuketi watu 19,000 ulionekana kuwa na takriban nusu ya idadi hiyo licha ya timu hiyo kudai kuwa zaidi ya watu milioni moja walikuwa wamejiandikisha kuhudhuria.

Timu ya Trump imedai kuwa takriban watu 12,000 walihudhuria kulingana na takwimu kutoka kwenye vifaa vya kiusalama vinavyokagua watu kwenye viingilio.

Wakati akitoa hotuba yake, Trump alishambulia mpinzani wake kutoka chama cha Demokratik Joe Biden akimtaja kuwa mwenye msimamo mkali wa mrengo wa kushoto huku akilaumu China kwa kuleta maambukizi ya virusi vya covid 19 nchini Marekani.

Meneja wa kampeni ya Trump Brad Parscale amesema huenda baadhi ya watu waliogopa kuhudhuria kutokana na kuwepo kwa “habari za uongo kwamba wangepata maambukizi ya covid19 au kujeruhiwa kwenye maandamano.”

-Imetayarishwa na Harrison Kamau, VOA, Washington DC.