Kampeni kubwa ya chanjo ya Polio imeanza Ukanda wa Gaza

Muuguzi akimpatia mtoto wa ki-Palestina matone ya chanjo ya polio huko Khan Yunis kusini mwa Ukanda wa Gaza. August 31, 2024.

Mamlaka zinapanga kuwapatia chanjo watoto katikati mwa Gaza kabla ya kuendelea na maeneo ya kaskazini na kusini

Mamlaka ya afya ya Palestina na mashirika ya Umoja wa Mataifa leo Jumapili yameanza kampeni kubwa ya chanjo dhidi ya polio katika Ukanda wa Gaza, wakiwa na matumaini ya kuzuia mlipuko katika eneo hilo ambalo limeharibiwa na vita vinavyoendelea kati ya Israel na Hamas.

Mamlaka zinapanga kuwapatia chanjo watoto kati-kati mwa Gaza hadi Jumatano kabla ya kuendelea na maeneo ya kaskazini na kusini mwa ukanda huo. Kampeni hiyo ilianza kwa idadi ndogo ya chanjo siku ya Jumamosi na inalenga kuwafikia watoto 640,000. Shirika la Afya Duniani (WHO) lilisema Alhamisi kuwa Israel imekubali kusitisha mapigano ili kufanikisha kampeni hiyo.

Kulikuwa na ripoti za awali za mashambulizi ya Israel katikati mwa Gaza mapema leo, lakini haikujulikana mara moja kama kuna mtu yeyote aliyeuawa au kujeruhiwa.