Serekali ya Somalia imeripoti kwamba kamanda wa kundi la Al Shabab, aliyeshiriki katika mashambulizi ya kundi hilo nchini Somalia, na Kenya, ameuwawa katika shambulizi la anga la Marekani, Desemba 17 karibu na mji wa Jilib.
Serekali imesema kwamba oparesheni iliyofanikisha kuuwawa kwa Maalim Ayman, ilikuwa ni matokeo ya ushirikiano baina ya vikosi vya taifa vya Somalia, na jeshi la Marekani. Katika taarifa iliyotolewa na wizara ya habari Alhamisi, imeeleza kwamba kuuwawa kwake ni mzigo ulioondolewa kwa watu wa Somalia.
Kamandi ya jeshi la Marekani barani Afrika, AFRICOM, imethibitisha kwamba shambulizi la Desemba 17 karibu na mji wa Jilib, lilimuua kamanda mmoja wa wanamgambo wa Al Shabab, na kusema kwamba hakuna vifo vya raia.
Kundi la wanamgambo wa Al Shabab, bado halijathibitisha mauaji ya mmoja wa makamanda wake wa juu.