Makamu wa Rais wa Marekani Kamala Harris alitangaza Jumamosi huko Dubai katika Mkutano wa Hali ya Hewa wa Umoja wa Mataifa COP28 kwamba Marekani inaahidi dola bilioni 3 kwa mfuko wa hali ya hewa ‘Green Climate Fund’ -- mfuko mkubwa zaidi wa hali ya hewa duniani ulioanzishwa kuzisaidia nchi zinazoendelea kushughulikia mabadiliko ya hali ya hewa.
“Duniani kote, kuna wale ambao wanataka kupunguza au kusitisha maendeleo yetu. Viongozi wanaokataa sayansi ya hali ya hewa, kuchelewesha hatua za hali ya hewa na kueneza habari potofu,” makamu wa rais alisema.
Ahadi hiyo ya mabilioni ya dola kwa mfuko wa hali ya hewa, hata hivyo, lazima kwanza iidhinishwe na Bunge la Marekani, ambalo limegawanyika juu ya mchango huo.
Pia Jumamosi, Marekani ilitoa ahadi ya kuondoa mitambo yote ya kuzalisha umeme kwa kutumia makaa ya mawe nchi ilipojiunga na Muungano wa Powering Past Coal Alliance. Makaa ya mawe ndio mchangiaji mkubwa zaidi wa mzozo wa hali ya hewa kwa mujibu wa muungano huo.
Tofauti kali ziliwekwa wazi Ijumaa katika mkutano wa COP28 kuhusu matumizi ya baadaye ya nishati mbadala.
Siku moja baada ya rais wa COP28, Sultan al-Jaber wa Umoja wa Falme za Kiarabu ambaye pia ni mkuu wa kampuni ya taifa ya mafuta ya UAE -- alifungua mkutano kwa wito wa kutoondoa kabisa bali kupunguza matumizi ya nishati ya makaa ya mawe, mafuta na gesi. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alitaka kinyume na hivyo.
Akiwahutubia wajumbe, Gutterres alisema, hatuwezi kuokoa sayari inayowaka kwa bomba la moto la mafuta ya nishati ya makaa ya mawe, mafuta na gesi na alitoa wito wa kuharakishwa kwa mabadiliko ya haki na ya usawa kwa nishati mbadala.
Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa alikuwa akizungumzia makubaliano ya hali ya hewa ya Paris ya mwaka 2015 ambayo yanataka juhudi za kupunguza ongezeko la joto duniani hadi nyuzi joto digrii 1.5 celsius juu ya viwango vya viwanda, akisema njia pekee ambayo lengo hilo linaweza kufikiwa ni iwapo dunia itaacha kuchoma nishati ya makaa ya mawe, mafuta na gesi. Si kupunguza.
Mizozo kuhusu matumizi ya nishati hiyo ilimsukuma mwanachama mashuhuri wa bodi ya ushauri ya COP28 kutangaza kujiuzulu Ijumaa.
Shirika la habari la Reuters limeripoti kuwa Rais wa zamani wa Kisiwa cha Marshall, Hilda Heine alijiuzulu katika barua aliyomwandikia Rais wa COP28 al-Jabar, akisema ripoti zinazodai UAE ilipanga kutumia mkutano huo kwa uwezekano wa kujadili kuhusu nishati ya vyanzo vya asili na mikataba mingine ya kibiashara zinakatisha tamaa na kutishia kudhoofisha uaminifu wa mchakato wa mashauriano ya pande nyingi.
Reuters inaripoti barua hiyo iliendelea kusema kuwa vitendo hivyo vinadhoofisha urais wa COP na mchakato kwa ujumla.
Mapema wiki hii BBC ikifanya kazi na Kituo cha Kuripoti Hali ya Hewa iliripoti nyaraka zilizovuja zikibaini mipango ya maafisa wa UAE kujadili mikataba ya nishati ya vyanzo vya asili na mataifa 15. Al-Jaber alikanusha vikali ripoti hiyo.
Pia siku ya Ijumaa, Mfalme Charles III wa Uingereza alihutubia mkutano huo akisema ulimwengu uko mbali sana na malengo yake ya hali ya hewa, alisema anaomba kwa moyo wake wote mkutano huo uwe hatua nyingine muhimu ya kuelekea mabadiliko ya kweli ya hali ya hewa.
Katika matamshi yake Ijumaa, Mfalme Abdullah II wa Jordan alihusisha mabadiliko ya hali ya hewa na mgogoro huko Gaza, akisema hawawezi kuzungumza juu ya mabadiliko ya hali ya hewa kwa kutengwa na majanga ya kibinadamu yaliyotuzunguka. Alisema maelfu wameuawa, kujeruhiwa au kukoseshwa makazi katika eneo lililo mstari wa mbele wa mabadiliko ya hali ya hewa, ambayo alisema inakuza uharibifu.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken, katika hotuba yake alihusisha mabadiliko ya hali ya hewa na mzozo wa chakula duniani, akitolea mfano takwimu zinazoonyesha mahitaji ya chakula duniani yanayokadiriwa kuongezeka kwa asilimia 50 ifikapo mwaka 2050, huku hali ya hewa ikitarajiwa kupunguza mavuno ya mazao kwa kiasi cha asilimia 30 katika kipindi hicho.
Wakati wa siku yake ya ufunguzi Alhamisi, mkutano huo walikubaliana na mfuko mpya wa dola milioni 420 kuyazsaidia mataifa maskini yaliyo hatarini kukabiliana na gharama ya majanga yanayosababishwa na mabadiliko ya hali ya hewa kama ukame mafuriko na kupanda kwa kina cha maji ya bahari.
Mjumbe wa hali ya hewa wa Marekani John Kerry aliyaita makubaliano hayo ni njia nzuri ya kuanza kwa mkutano huo.
Mpango huo wa siku moja unaweza kufungua njia kwa makubaliano zaidi katika COP28.
COP inasimamia Mkutano wa wanachama kwa ajili ya Mkataba wa awali wa Mfumo wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya hali ya hewa. Kwa sasa kuna washiriki 198 kwenye mkutano huo.
Mkutano wa COP wa sasa unaendelea hadi Desemba 12.