Makamu Rais wa Marekani Kamala Harris anatarajiwa kukutana na mjumbe wa baraza la mawaziri la vita la Israel, Benny Gantz huko White House leo Jumatatu, siku moja baada ya kutoa wito wa kusitisha haraka mapigano huko Gaza.
Afisa mmoja wa White House amesema mazungumzo hayo yanatarajiwa kulenga vifo vya raia wa Palestina, kupata sitisho la mauda la mapigano, na kuachiliwa mateka pamoja na kuongeza misaada katika eneo hilo.
Makamu Rais ataelezea wasiwasi wake juu ya usalama wa watu milioni 1.5 huko Rafah, afisa huyo alisema, akiongeza kuwa Israeli ina haki ya kujilinda kutokana na vitisho vya kigaidi vya Hamas.
Katika taarifa yake, Gantz alithibitisha kuwa atakutana na Harris, pamoja na mshauri wa usalama wa taifa wa White House, Jake Sullivan pamoja na wabunge wa Republican na Democratic.