Tangazo la Deby limekuja mwishoni mwa wiki iliyoshuhudia ghasia kufuatia kupigwa risasi na kuuwawa kwa mwanasiasa wa upinzani Yaya Dillo, kwenye mji mkuu wa N’Djamena. Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, kifo cha Dillo cha Jumatano kilichozua utata kimefichua migawanyiko miongoni mwa viongozi wa kisiasa, wakati huu muhimu ambapo taifa hilo la Afrika ya Kati limeahidi kurejesha demokrasia kwa njia ya upigaji kura.
Wakati akitoa hotuba mbele ya maafisa pamoja na wafuasi wake, Deby ametangaza kuwania kwake bila kutaja ghasia zilizoshuhudiwa hivi karibuni. Mwanzoni Deby aliahidi miezi 18 ya mpito kuelekea kwenye uchaguzi, baada ya kuchukua usukani 2021, kufuatia baba yake Rais Idriss Deby kuuwawa akiwa kwenye uwanja wa vita dhidi ya waasi.
Hata hivyo baadaye serikali ilifikia mapendekezo ambayo yangechelewesha uchaguzi hadi mwaka huu, wakati akiruhusiwa kisheria kushiriki zoezi hilo. Ijumaa serikali ya Deby ilithibitisha kuwa mjomba wake Jenerali Saleh Deby Itno alikuwa amekamatwa kufuatia ghasia za Jumatano. Itno hivi karibuni alihamia chama cha upinzani cha marehemu Dillo cha Socialist Party Without Borders.