Ameonya kwamba juhudi za kijeshi DRC zitafeli, namna zilivyofeli miaka 10 iliyopita, M23 waliposhambuliwa na wanajeshi wa Tanzania, akisema kwamba waliotuma wanajeshi walikosa kufuata ushauri wake.
Kagame amesema kwamba swala la ukosefu wa usalama mashariki mwa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo sio la kijeshi na haliwezi kusuluhishwa kwa silaha bali ni swala la kisiasa ambalo linastahili kushughulikiwa kwa kusaidia serikali ya DRC, akionya kwamba siku yoyote kombora litaanguka Rwanda kutoka DRC, ataingia nchi hiyo Jirani kwa vita, na “aliyerusha kombora atakosa usingizi”.
Akihutubia mawaziri na viongozi wa serikali, Kagame amesema kwamba amesikia kila mara baadhi ya viongozi wakisema kwamba mipaka ya DRC lazima iheshimiwe, jambo analokubaliana nalo, lakini vile vile ni lazima mipaka ya Rwanda iheshimiwe.
“Hakuna hata siku moja… siku moja… ambayo ninajua… labda wewe unajua… ambayo hawa wanajeshi waliwahi kupigana na FDLR, kujaribu kuwaondoa lakini wamekuwa wepesi na makini kupigana na M23. Hilo ndilo lililofanyika mwaka 2012. Na tuliwaonya, tulikuwa tukiwaonya kwamba mnashughulikia jambo ambalo ni nusu ya shida na nusu nyingine itarugi kutusumbua sote.”
Ameeleza kughadhabishwa kila mara na lawama zinazoelekezwa kwa Rwanda kutokana na matatizo yaliyo DRC, akisema kwamba swala la waasi wa M23 sio swala la Rwanda na hakuna namna anaweza kuajibika nalo.
“Kuna zaidi ya makundi 100 ya waasi mashariki mwa Congo. Haiwezikani kwamba yote yanafadhiliwa na Rwanda. Ingekuwa kwamba Rwanda ndiye mfadhili wao, pengine yangekuwa yameungana.”
Madai ya Rwanda kufadhili waasi ili kuiba madini ya DRC
Kagame, amesema wanaoshutumu Rwanda kwamba inaiba mali ya Congo ni wanafiki wakubwa akiongezea kwamba kwa vitu vyote ambavyo Rwanda haiwezi kuhesabiwa ndani ni wizi.
“Tunafanya kazi kwa bidi kupata tulichonacho na tunachopata. Tupo mahali tulipo na tumepiga maendeleo mema kwa sababu ya bidii yetu na hata hizi nchi zenye nguvu duniani zinazotushutumu kwa mambo hatujui, huwa wanatusaidia sana. Wakichunguza hayo madai, hawatapata mahali popote pengine ambapo pesa wanayotoa inatumika vyema kuliko Rwanda. Kwa kila dola wanayotupatia, tutawaonyesha kazi kubwa ambayo imefanya kuliko mahali kwingine ambapo huwa wanapeleka pesa yao.” Amesema Kagame akiongezea kwamba
“Wanadai kwamba sisi tunaiba mali yao. wanasema Tunaiba madini yao, dhahabu yao….niliuliza hao viongozi kwamba kuna kitu ninachojua…kuna watu huwa wanatoka Congo na madini na wanapitia hapa wakienda Dubai, Brussels, Tel Aviv, Russia… nikawauliza, je mpo kwenye orodha ya wale wanaoiba madini ya Congo? Je, mbona hamzungumzii pale madini hupokelewa? Na tukishughulikia hili swala la vita na kumaliza, wakose kupata dhahabu, tena kutakuwepo matatizo zaidi. Watatushutumu. Tufanye nini sasa jameni?”
Kama unatafuta mtu anajua vita, kuja kwangu nitakuonyesha - Kagame
Kuhusu matamshi ya rais wa Jamhuri wa kidemokrasia ya Congo Novemba 2022, alipohutubia taifa kwamba diplomasia ilionekana imefeli na kwamba kuna uwezekano wa DRC na Rwanda kuingia katika vita, Kagame bila kumtaja Tshisekedi na badala yake kumtambua kama ‘mtu huyo’, amesema kwamba “kama unatafuta mtu anayejua kitu kuhusu vita, kuja kwangu tafadhali. Najua kitu kuhusu vita.”
Kagame amedai kwamba rais wa DRC Felix Tshisekedi inajaribu kuunda mazingira ya kuwepo hali ya vurugu ili uchaguzi usifanyike na apate fursa ya kuendelea kukaa madarakani.
“sio kwamba alishinda uchaguzi wake wa kwanza jinsi tunavyojua. Kama anajaribu kutafuta njia nyingine ya kuahirisha uchaguzi ujao, basi atumie sababu zingine lakini sio Rwanda. Kutafuta matatizo na Rwanda hakutaeta kura.”
Amesisitiza kwamba ni aibu kubwa kwa wahusika wote katika mgogoro wa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo kwamba wameshindwa kusuluhisha mgogoro huo licha ya kuwa wengi, kuwa na raslimali, na ambayo ni rahisi kusuluhisha.
“wanapapasa tatizo na kulaumu kila mtu isipokuwa wao. Ni jambo la kuhuzunishwa kwamba kwenye orodha hiyo fupi nimetaja ya wahusika, nchi na wengineo, imekuwa rahisi kwamba Rwanda ndio inalaumiwa sana kutokana na matatizo ya Congo. Kila mara, Rwanda ndio mhusika na mwanzilishi wa matatizo ya Congo. Sio FDLR, sio serikali ya Congo ambayo inastahili kuajibika kwa matatizo yake na watu wake, sio umoja wa mataifa, sio nchizenye nguvu zaidi duniani hasa Marekani, Uingereza, Ufaransa, ni Rwanda tu kila mara.”
“Huenda hatuna namna lakini tuna mbinu. Msitudharau”
Kagame anasema kwamba nchi yake huenda ikachukuliwa kama haina “namna lakini ina mbinu” ndio maana kw akulinganisha Rwanda na Congo kuna mengi ambayo Congo inatoa kwa “watu hao wanaoilaumu Rwanda kuliko kile ambacho Rwanda huwa inawapatia.”
“Watu hawa lazima wawe waangalifu wanaposhughulikia matatizo ya Congo. wanaonekana kwamba ni Lazima wasaidie Congo ili kuongeza machungu yao na Wakongo waendelee kulaumu mtu mwingine kwa matatizo yake. Mahali rahisi pa kuweka lawama zao ni Rwanda.”
Amelinganisha Rwanda na matawi ya ndizi ambayo yeyote anayetaka kutumia, anakata yaliyo chini. Akiongezea kwamba “wanajidanganya” na kwamba “sisi kwa ufupi wetu, hatuna namna lakini tuna mbinu na tupo imara ambayo huwajajua, na hawawezi kuelewa namna tulivyo imara. Na wanaofikiria kwamba wanaweza kuendela kukata majani yetu kwa sababu sisi ni wafupi, mmejidanganya.”
Kagame amshutumu kundi la FDLR mara kadhaa, akisema wana washirika wao, wakiwemo watu ambao wanazuiliwa katika magereza ya Rwanda walioletwa kutoka nchi za nje, akiwa na maana akiwemo Paul Rusesabagina anayetumikia miaka 25 gerezani kwa makosa ya ugaidi kwa kile ambacho serikali ya Rwanda inadai kwamba alikuwa anaunga mkono kundi la waasi lililotekeleza mashambulizi nchini Rwanda mwaka 2018 na 2019.
Rusesabagiza alikuwa mkosoaji mkubwa wa rais Kagame, lakini ukosoaji wake alikuwa anafanya akiw auhamishoni.
Baadhi ya wachambuzi walikuwa wanamuona Rusesabagina mwenye umri wa miaka 67 kuwa mpinzani mkubwa wa rais Paul Kagame katika uchaguzi mkuu.
“Wapinzani tumewaacha wazunguke waingie kwa makosa”
Kando na watu Kagame amesema wanazuiliwa gerezani, ametaja pia “wengine wanaozunguka hapa na pale wakijiita wanasiasa wa upinzani, ambao tumewaacha tu wajiingize kwa makosa wenyewe wakati mwafaka, itakapohitajika kuwashughulikia, na tutawashughulikia.”
Kagame anasema kwamba tatizo la FDLR limekuwepo kwa karibu miaka 30 kwa kile anachoamini kwamba kuna watu mahali wanataka tatizo la waasi wa FDLR liendelee kuwepo kwa muda mrefu, waendelee kusumbua Rwanda.
Ameeleza kukasirishwa kila mara na wanaodai kwamba serikali yake inakandamiza haki za kibinadamu na kila aina ya shutuma dhidi yake.
Amedai kwamba wanasiasa wa upinzani wana uhusiano na kundi la waasi la FDLR na waliohusika na mauaji ya kimbari, na kwamba wengi wao wapo huru nje ya Rwanda kwa sababu nchi zimekataa kuwarudisha Rwanda ili wafunguliwe mashtaka kwa madai kwamba Rwanda haiheshimu haki za kibinadamu, uhuru wa kujieleza na sheria.