Kagame amesema kwamba wanajeshi wake wameshika doria kwenye mpaka wa Rwanda na DRC.
“Mashambulizi yanayofanywa na kundi la FDLR yamepelekea sisi kuchukua hatua na kutuma idadi kubwa ya wanajeshi kwenye mpaka na Congo,” amesema Kagame katika kikao na waandishi wa habari mjini Kigali.
FDLR ni kundi la wapiganaji waliokuwa wanajeshi wakati wa utawala wa Rwanda, ulioangushwa na rais Paul Kagame. Wanatuhumiwa kwa kusababisha mauaji ya kimbari nchini Rwanda mwaka 1994.
Rwanda inadai kwamba FDLR wanapewa ulinzi na msaada na serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, na kwamba wapiganaji hao ni hatari kwa usalama wa Rwanda.
“Kile ambacho tunahitaji kufanya, tutafanya inapohitajika. Hakuna mtu atakayevuka mpaka wetu na kuwashambulia watu wetu au kutumia sehemu yoyote iliyo karibu na mpaka wetu kutekeleza mashambulizi ndani ya Rwanda. Atakabiliwa inavyostahili,” ameonya Kagame akiongezea kwamba “hii siyo siri na tumesema hadharani.”
Vyombo vya habari vya Uganda na Rwanda vimeripoti kwamba Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo nayo imetuma wanajeshi wake kwenye mpaka na Rwanda.
Hii ni mara ya pili mwaka huu, rais Kagame ametishia kuivamia DRC kijeshi iwapo Rwanda itashambuliwa.
Mnamo mwezi Januari, rais Kagame alisema kwamba hataiangalia FDLR tu ambao wanaendelea kutishia usalama wa Rwanda.
“Nitawapa sababu ya kunilaumu. Tumejiandaa kulaumiwa, lakini tutalaumiwa kwa kufanya kile tunachostahili kufanya.” Alisema Kagame mapema mwaka huu.
Mgogoro kati ya Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo umeongezeka kufuatia mapigano ya kundi la waasi la M23.
Msaada kwa waasi wa M23 na wa FDLR
DRC inailaumu Rwanda kwa kuunga mkono waasi wa M23, madai yanayoungwa mkono na ripoti ya wataalam wa Umoja wa Mataifa na watafiti wengine. Rwanda imekanusha madai na ripoti hizo.
“Kundi la M23 lilianza mwaka 2012. Walijaribu kutumia nguvu za kijeshi kutatua shida hiyo. Wengine walikimbilia Uganda, wengine Congo na wengine walikimbilia hapa. Makubaliano yamefanyika kuhusu hatua za kuchukua kumaliza mgogoro huo tangu mwaka 2012 lakini makubaliano hayo yamepuuzwa hadi mapigano yalipoanza tena. Kuna zaidi ya makundi yenye silaha 120 mashariki mwa DRC, M23 ni moja tu ya kundi hilo. Sijasikia hata wale wanaoichukia Rwanda, wanaosema uongo kuhusu Rwanda wakisema kwamba Rwanda inahusika katika kuunda hayo makundi yenye silaha. Wanachofanya ni kutulaumu kwamba tunashirikiana na kundi la M23. Nani aliunda yale makundi mengine zaidi ya 100 yenye silaha na kwa nini?”
Kwa upande mwingine, ripoti ya Umoja wa Mataifa inasema kwamba DRC inaliunga mkono kundi la wapiganaji la FDLR, madai ambayo serikali ya Kinshasa inayakanusha.
“FDLR wameingizwa katika jeshi la Congo FARDC na serikali ya DRC inajua hilo vizuri sana. Walishambulia kaskazini mwa Rwanda.” Amesema Kagame.
Kagame amesema kwamba DRC haijachukua hatua yoyote kumaliza tatizo la FDLR lakini inaendelea kuilaumu Rwanda kwa kuwasaidia wapiganaji wa M23.
“Kwa sababu gani Rwanda iingie DRC au kuliunga mkono M23? Kundi la FDLR linafanya nini DRC? Mbona FDLR wanashirikiana na serikali ya Congo? Mbona wapo Congo? Rwanda inastahili kufanya nini? Tuendelee kunyamaza wakati FDLR wanavuka mpaka na kuua watu wetu?” ameuliza Kagame.
Kiongozi huyo wa Rwanda ameendelea kuuliza maswali kadhaa. “Wanajeshi wa MONUSCO na wale wengine ambao wamekwenda huko kuleta amani wamefanya kazi gani DRC? Kuwapa silaha FDLR? Lazima mtu ajibu maswali hayo.”