Kagame: Rwanda inaathirika kutokana na matatizo ya kisiasa ya DRC

Rais wa Rwanda Paul Kagame

Rais wa Rwanda Paul Kagame, ameuambia mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa unaoendelea mjini New York, Marekani kwamba matatizo ya usalama yanayoikumba Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ni ya kisiasa, na kwamba yanahitaji suluhu ya kisiasa.

Katika hotuba ya dakika 7, ambayo ametoa saa chache baada ya kushutumiwa na rais wa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo Felix Tshisekedi, Kagame hakuzungumzia sana shutuma zilizoelekezwa kwa nchi yake, badala yake ameangazia namna matatizo yanayokumba ulimwengu kwa jumla yanaweza kusuluhishwa.

Anataka viongozi wote duniani wakiongozwa na Marekani kuhakikisha kwamba kuna rasilimali za kutosha kuimarisha mfumo wa afya, viongozi kushirikiana kuhakikisha kwamba kuna uwekezaji wa kutosha katika kubuni nafasi za ajira ili kukabiliana na wimbi la uhamiaji na kukabiliana na makundi ya wapiganaji yenye misimamo mikali.

Kagame amesema kwamba kulaumiana na kushutumiana kuhusu matatizo yanayoikabili duniani sio hatua ambayo itasuluhisha matatizo yanayoikumba dunia.

“Katika sehemu za Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo hali ya usalama ya sasa inaonyesha kwamba hakuna mabadiliko yametokea katika miaka 20 iliyopita licha ya kuwa na jeshi kubwa la kulinda amani la Umoja wa Mataifa lilipoingia nchini humo. Hali hiyo imeiweka nchi Jirani katika hatari ya kiusalama hasa Rwanda kutokana na mashambulizi ya mpakani yanayoweza kuzuiliwa. Kuna haja ya haraka sana kutafuta suluhu ya kisiasa kuhusu hali ya usalama nchini DRC.” Amesema Kagame.

Mchakato wa amani wa Jumuiya ya Afrika mashariki

Amezungumzia kwa kifupi sana hatua ya viongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kuunda jeshi la pamoja kuisaidia DRC, ambayo ameyataja kuwa ‘mchakato wa Nairobi’ kwamba unaweza kuisaidia kusaidia Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Jeshi la Jumuiya ya Afrika Mashariki linatarajiwa kuingia Mashariki mwa DRC kupigana na zaidi ya vikundi 100 vya waasi katika sehemu hiyo.

Akihutubia kikao hicho Jumanne, rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Felix Tshisekedi amesisitiza kwamba Rwanda inatoa msaada kwa waasi wa M23 wanaopigana vita Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo.

Tshisekedi ameutaka Umoja wa Mataifa na ulimwengu kwa jumla kuchukua hatua za dharura na kali kuiwajibisha serikali ya Rwanda, akisema ndio inachangia pakubwa kuvuruga amani Mashariki mwa DRC.

Tshisekedi ameiambia Umoja wa Ulaya kwamba licha ya Rwanda kutajwa kila mara katika vita vya DRC, inaendelea kutoa silaha na msaada wa kijeshi kwa kundi la waasi la M23 na kukiuka mikataba yote ya kimataifa pamoja na maamuzi ya Umoja wa Afrika, Jumuiya ya Afrika Mashariki na SADC.

Katika hotuba iliyojaa ushawishi na kuilenga Umoja wa Mataifa moja kwa moja, mbele ya viongozi wengine kutoka kote duniani kwenye kikao ya 77 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York, rais Tshisekedi ameulenga utawala wa rais wa Rwanda Paul Kagame, na kuueleza ulimwengu namna nchi hiyo, jirani wa DRC inavyovuruga usalama katika majimbo ya Mashariki ya Ituri, Kivu Kaskazini na Kivu Kusini, katika vita ambavyo vimedumu kwa zaidi ya miaka 20.

“Rwanda ndiye mhusika mkubwa katika vita nchini mwangu”

Tshisekedi, amesisitiza kwamba wakati ulimwengu unapambana na ugaidi na vita vingine, majirani wa DRC ikiwemo Rwanda wanayaunga mkono makundi ya waasi wakiwemo waasi wa M23 kuipiga vita serikali ya DRC, hawaheshimu mfumo wa sheria, hawaheshimu mpaka wa DRC, na wanaiba mali za DRC.

Isitoshe, licha ya kuwepo juhudi za Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika, Jumuiya ya Afrika Mashariki, Umoja wa Ulaya, muungano wa SADC, miongoni wa washirika wengine kutafuta suluhu ya kudumu nchini DRC, Rwanda imekataa kuheshimu juhudi hizo.

Ameishitaki Rwanda moja kwa moja kwa Umoja wa Mataifa, akisema inawaunga mkono waasi wa M23 kwa kuwapa silaha na msaada wa kijeshi, na hata kuua wanajeshi wa Umoja wa Mataifa.

“Kundi la waasi la M23 likisaidiwa na Rwanda hata lilipiga na kuiangusha ndege ya jeshi la amani la Umoja wa Mataifa MONUSCO na kuua wanajeshi 8. Kwa kufanya hivyo, walitenda uhalifu wa kivita.”

Rais Tshisekedi ameeleza juhudi zote ambazo DRC imechukua kuleta amani Mashariki mwa DRC lakini zimefeli, akiwalaumu majirani zake. Miongoni mwa juhudi hizo ni kusaini mikataba ya amani, ikiwemo ile ambayo imesimamiwa na jumuiya ya kimataifa, kikanda na Umoja wa Afrika lakini ilivunjika baada ya miezi michache ya kusainiwa.