Kagame: kuna watu wanataka kuipindua serikali yangu kwa kuwaunga mkono FDLR huku wakiwaondoa M23.

Rais wa Rwanda Paul Kagame akihutubia wangune mjini Kigali Jan 9, 2023

Rais wa Rwanda Paul Kagame amesema kwamba kundi la waasi la Democratic Forces for Liberation of Rwanda - FDLR, linaloshutumiwa na serikali ya Rwanda kwa kusababisha mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 linaungwa mkono na baadhi ya watu kwa lengo la kuipindua serikali yake.

Bila ya kutaja majina ya nchi au watu anaodai kwamba wanaliunga mkono kundi la FDLR, Kagame amedai kwamba kundi hilo linajificha katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC.

Kagame amesema hayo wakati akiwahutubia maseneta. Video ya hotuba hiyo imewekwa kwenye akaunti rasmi ya You Tube, ya rais Kagame – Paul Kagame.

“Kundi la FDLR ambalo limepewa hifadhi kwa miongo kadhaa. Nadhani limehifadhiwa makusudi. Kwa FDLR na makundi mengine yenye ushirikiano nalo kuwa huko (DRC) kwa miongo kadhaa, haiwezi kuwa bila sababu maalum, haiwezekani,” amesema rais Kagame.

“Unaposema kwamba waasi wa M23 na watu wengine ambao unawaondoa – ukisema warudi Rwanda kwa hiari au bila hiari, lakini huzungumzii kuhusu kundi la FDLR kwa sababu unalitaka kuendelea kuwepo….. hiki ndio kiini cha mzozo,” ameongezea kusema Kagame.

“Huo ndio utakaso unaozungumziwa. Unataka kuliondoa kundi moja na kuliachajlingine unalopendelea. Lakini kitu kingine ni kwamba FDLR na makundi mengine unayoyasikia yanafanya hizi kelele zote. Kuna watu wanadhani kwamba wanajaribu kutafuta mbinu mbadala tofauti na ilivyo Rwanda.”

Kundi la FDLR linajumuisha waliokuwa wanajeshi wa serikali ya Rwanda, iliyokuwa madarakani kabla ya kupinduliwa na waasi wa RPF lililoongozwa na rais Paul Kagame, mwaka 1994.

FDLR, wengi wao kutoka kabila la wahutu wanashutumiwa kwa kusababisha mauaji ya Watutsi Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

'FDLR ni sehemu ya jeshi la DRC'

Ripoti ya wataalam wa Umoja wa Mataifa kuhusu vita vya Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, inasema kwamba waasi wa FDLR wanashirikiana na jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na kushirikiana kupigana na waasi wa kundi la M23.

Ripoti hiyo pia inasema kwamba Rwanda inawaunga mkono waasi wa M23, madai ambayo serikali ya Kigali imekanusha mara kadhaa.

Serikali ya Rwanda imewashutumu waasi wa FDLR kwa kuvuka mpaka na kusababisha mashambulizi ndani ya Rwanda, na kupelekea vifo vya raia.

Rais Paul Kagame amedai kwamba kuna watu wenye nia ya kutekeleza mapinduzi nchini Rwanda.

“Unajua kuna hilo jambo. Unapoona mambo haya yakifanyika, ni kama… hapana, tumechoka na serikali ya Rwanda. Kwa hivyo wanataka akina Kagame na serikali yake ya RPF kuondoka madarakani. Wanasema kwamba Rwanda haina uhuru, hakuna uhuru wala demokrasia, lakini wao ndio wananinyima uhuru. Raia wa Rwanda wamenyimwa uhuru wao. Hiyo ndio sababu watu wanajaribu kujitafutia njia mbadala,” amesema Kagame huku akiyashutumu makundi ya kutetea haki za binadamu kwa kuukosoa utawala wa wake.

“Wewe ni nani wa kuwaamulia watu namna wanavyostahili kuishi au kuamua tabia zao? Huwezi kunifunza namna ninavyostahili kuishi au tabia zangu. Hata mimi sipendi tabia zako. Kwa hivyo unapata wapi mamlaka ya kuniambia namna ninavyostahili kuishi na kufanya mambo yangu? Wewe ni nani? Unatoka wapi? Unaniambia nini?” amesisitiza Kagame huku wabunge wakimpigia makofi.

Wanajeshi wa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo wakipiga doria katika mji wa Rutshuru mashariki mwa DRC.

Tumeona ya kutosha, hatutaki upumbavu. Ukinishambulia, tutapigana

“Kwa hivyo, ningependa kuwaambia, wale wanaodhani kwamba wanaweza kubadilisha haya, tumeona ya kutosha katika historia yetu. Hatutaki tena mambo ya upumbavu. Lakini ninachowaahidi, wale walio na umri sawa na wangu, hata wale ambao umri wao ni wa chini ukilinganishwa na wangu, wale wenye miaka 50 na wanaotaka kutekeleza mapinduzi ya utawala, mtakuwa wazee na kuondoka duniani, bila kuona hayo mabadiliko mnayotaka,” amesema Kagame bila kueleza anaozungumzia, wenye umri wa chini ya miaka 50.

Kwa kuwalinganisha na marais wenzake katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, rais wa Kenya Dr. William Ruto ana umri wa miaka 56, Evariste Ndayishimiye wa Burundi ana umri wa miaka 54, Felix Tshisekedi 59, Paul Kagame 65, Yoweri Museveni 78 na Salva Kiir ana umri wa miaka 71.

Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki zimekubaliana kutuma wanajeshi wake mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kupambana na makundi ya waasi likiwemo kundi la M23 linalodaiwa kuungwa mkono na serikali ya Rwanda.

Kenya na Burundi tayari zina wanajeshi wake mashariki mwa DRC wakishirikiana na wanajeshi wa DRC. Sudan Kusini imetuma wanajeshi 750. Uganda imeahidi kutuma wanajeshi lakini hakuna tarehe maalum imetangazwa na mtoto wa rais wa Uganda Yoweri Museveni amesema kwamba wanajeshi wa Uganda hawatapigana na waasi wa M23.

Wanajeshi wa Kenya wanaongoza oparesheni hiyo na tayari wamefanikiwa kuwaondoa waasi wa M23 katika baadhi ya sehemu ambazo wamekuwa wakishikilia kwa muda.

Waasi wa M23 walikabidhi kambi ya jeshi ya Rumangabo, iliyo mashariki mwa Kivu Kaskazini, kwa wanajeshi wa Kenya. Waasi wameondoka katika mji huo wa Rumangabo ambao wamekuwa wakiushikilia tangu mwezi Oktoba.

Waasi hao pia wameondoka Kibumba, japo ripoti ya Umoja wa Mataifa inasema kwamba bado wapiganaji wake wapo Kibumba.

Ripoti hiyo ya wataalam wa Umoja wa Mataifa vile vile inadai kwamba waasi wa M23 wanajiimarisha katika sehemu nyingine mashariki mwa DRC.

“Nataka kuwahakikishia kwamba nchi hii imepitia mengi, na nimeona mengi. Matokeo yake yote ni kwamba sisi ni kama mwamba. Wale wote wanaojiingiza katika michezo ya kutuchezea, wanafanya mzaha, na tunaweza kuendelea kufanya mzaha. Ukinishambulia, tunapigana – nitapigana. Kama unataka tufanye kazi pamoja, tutashirikiana. Tunaweza kuwa marafiki wazuri sana na watu. Lakini pia, hatuwezi kuwa watu wazuri kwa wale wanaotaka kuwa maadui wetu.”

TKambi ya wakimbizi ya Mahama nchini Rwanda Rwanda.

Rwanda kuwafukuza wakimbizi kutoka DRC

Rais Kagame amesema kwamba Rwanda imekuwa ikiwapokea wakimbizi kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kwa zaidi ya miaka 20, na kwamba ni ‘aina moja ya watu’.

“Kuna kundi moja la wakimbizi ambalo nadhani hatutaruhusu kuwapokea. Hatuwezi kuendelea kutoa makazi kwa wakimbizi wanaokuja kwa sababu ya utakasaji wa kijamii katika nchi nyingine na kuwa sehemu ya kutupa watu hao ambao wananyimwa haki zao,” amesema rais Kagame.

“Wakati tulikuwa bado na uhusiano mzuri na rais wa sasa wa DRC, nilizungumzia swala hili alipoingia tu madarakani. Nilimwambia kwa kirefu kuhusu swala la wakimbizi likiwemo namna ya kumaliza swala la wakimbizi likiwemo kuwafanya kuwa raia wa Rwanda na hata kuhatarisha maisha yao, kama njia ya kusuluhisha tatizo hilo. Nilimwambia pia kuhusu ugumu wa kutekeleza pendekezo hilo. Wakimbizi hao hawataki uraia tuliokuwa tunapendekeza kwa sababu wanataka kurudi nyumbani kwao DRC.”

Kagame amesema kwamba serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imeendelea kuishutumu Rwanda kwa matatizo hayo ikiwemo kuliunga mkono kundi la waasi la M23, na kwamba waasi hao warudi mahali walipotoka.

Amesema kwamba Rwanda imejaribu kutoa maelezo ya kutosha kila mara kwamba waasi wanaopigana mashariki mwa DRC hawakutoka Rwanda.

“Wanaotoa madai hayo wanasema kwamba hawa ni Watutsi kutoka Rwanda, hata kama ilikuwa miaka 100 iliyopita, na kwamba lazima warudi Rwanda. Hivyo ndivyo serikali ya Rwanda inavyosema. Sijui wanaounga mkono wazo hilo wakiwa nje ya nchi hizo wanajua hilo na kwamba pia wanaliunga mkono maksudi kwa kujua wanachofanya, lakini ni ukiukaji mkubwa wa ahaki za watu na ukiukaji wa kanuni za nchi yetu.”

Kagame amesema kwamba Rwanda haitaendelea kubeba mzigo wa matatizo yanayoendelea Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

“Hii siyo shida ya Rwanda. Na tutahakikisha kwamba kila mtu anaelewa kwamba hii siyo shida ya Rwanda. Tunaanza kwa kusema kwamba wale wanaodhani kwamba ni shida ya Rwanda na wala siyo ya Congo, kwanza ondoeni hawa raia wa Congo kutoka hapa. Hawa wanaoingia Rwanda kila siku kama wakimbizi kwa sababu nchi yao sio thabithi. Hilo siyo jukumu langu!” amesema Kagame akionekana mwenye hasira katika kikao cha bunge kilichojaa ukimya kando na kupigiwa makofi. “Haya ninayosema ni kwa ajili ya jumuiya ya kimataifa. Nakataa kwamba Rwanda inastahili kubeba huu mzigo na kuendelea kushutumiwa na kulaumiwa kila siku. Wabebeni na mpeleke kule mnataka au warudishe Congo na muwape ulinzi dhidi ya serikali yao na mamluki.”

Waasi wa M23 wakiwa karibu na mji wa Kibumba, mashariki mwa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, Dec. 23, 2022.

Ripoti za wataalam wa Umoja wa Mataifa kuhusu vita vya DRC

Rais Paul Kagame amekosoa ripoti za wataalam wa Umoja wa Mataifa akisema zinaandika sana kuhusu Rwanda badala ya kuangazia kuhusu yayotekelezwa na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

“Sio tu kwamba wanaeneza ujumbe wa chuki kati ya watu. Wanaua watu! Hadi sasa tunapokea wakimbizi wanaovuka mpaka na kuingia Rwanda na nina uhakika bado wataendelea kuvuka mpaka na kuingia Rwanda. DRC wanaiambia Umoja wa Ulaya, Marekani na wengine kwamba lazima mchukue hizi hatua dhidi ya Rwanda…. Mfanye dhidi ya Rwanda kwa sababu gani? Rwanda imefanya nini? Tumefanya nini? Kile tumefanya, ni lazima kwanza muelewe ni kwa sababu gani tungekuwa tunalifanya. Kwa sababu gani tungekuwa tunafanya lile mnatushutumu kwamba tumefanya? Mbona watu wasipate suluhu kwa hilo ambalo linatufanya kufanya hilo mnalotushutumu.”

Ametoa mfano akisema kwamba waasi wa FDLR walipovuka mpaka na kufanya mashambulizi ndani ya Rwanda, sehemu ya Kiningi, alishutumiwa na jumuiya ya kimataifa kwa kuchukua hatua kuwashambulia, akisisitiza kwamba endapo tukio kama hilo linatokea, atachukua hatua na “nitawapa sababu kamili ya kunilaumu. Tupo tayari kulaumiwa.”

Kagame amesisitiza kwamba Rwanda ipo tayari kukabiliana na maadui wake.

“Nimesikia kwamba kuna mamluki. Ukisikia kwamba nchi ina mamluki, jua kwamba hali ni mbaya sana. ikija kuhusu swala la kukabiliana na mamluki, tuna silaha za kutosha zaidi ya inavyohitajika. Mamluki ndio watu hawana maana kabisa unaoweza kutegemea. Hizo nchi zinazotegemea mamluki, jua kwamba mpo katika matatizo makubwa. Nasema haya kwa sababu yananikasirisha,” amesema rais wa Rwanda Paul Kagame.