Kagame kugombea mhula mwingine madarakani mwaka ujao

Rais wa Rwanda Paul Kagame April 22, 2014

Rais wa Rwanda Paul Kagame amesema kwamba atagombea mhula mwingine madarakani katika uchaguzi mkuu wa mwaka ujao.

Kagame, ambaye aliingia madarakani mwaka 2000, anaruhusiwa kisheria kugombea mhula mwingine madarakani kufuatia mabadiliko ya katiba yam waka 2015 yaliyopelekea kubadilisha kwa kizuizi cha mhula kwa rais.

Katika mahojiano yaliyochapishwa jumanne na jarida la kifaransa la Jeune Afrique, Kagame amesema kwamba ana furaha kwamba raia wa Rwanda wana Imani na uongozi wake na kwamba ataendelea kuwatumikia kadri ya uwezo wake.

Amethibitisha kwamba atagombea mhula mwingine katika uchaguzi ujao.

Kagame alishinda uchaguzi mkuu wa Agosti mwaka 2017 kwa asilimia 98.63 ya kura na kumpa mhula wa miaka 7 madarakani.

Amesifiwa kwa kuleta Amani na maendeleo ya uchumi nchini Rwanda tangu kutokea mauaji ya kimbari mwaka 1994, ambapo karibu watu 800,000 wengi wao kutoka kabila la watutsi waliuawa.

Hata hivyo, ameshutumiwa kwa ukiukaji mkubwa wa haki za kibinadamu, uhuru wa kisiasa na vyombo vya habari, madai ambayo amekanusha mara kadhaa.