Taarifa ya Rais iliotolewa Ijumaa imesema Tshibala anatokea kwenye chama kikubwa cha upinzani nchini DRC, kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters.
Hata hivyo habari hizo zimesema kuwa uteuzi huo unaweza kuwagawanya wapinzani wa Kabila baada ya mazungumzo yaliomtaka aondoke madarakani kuharibika wiki iliopita.
Pia imemtaja Tshibala kuwa ni waziri mkuu katika serikali ya mpito ambayo itakuwa na jukumu la kuandaa uchaguzi wa rais ifikapo mwisho wa mwaka baada ya Kabila kukataa kuachia madaraka muda wake ulipomalizika Disemba mwaka jana.
Chini ya makubaliano yaliofanyika Disemba, Kabila anaweza kuendelea na madaraka mpaka uchaguzi mwengine utakapofanyika mwisho wa mwaka.
Lakini mazungumzo ya kutekeleza makubaliano yaliyofikiwa yalivunjika wiki iliopita na kuteuliwa kwa Tshibala inakadiriwa kuwa bila shaka utazidi kudhoofisha juhudi za kumfanya Kabila aheshimu makubaliano hayo.
Tshibala alifukuzwa kutoka Chama cha upinzani kikubwa kuliko vyote UDPS, mwezi uliopita baada ya kupinga uteuzi wa watakao chukua nafasi ya kiongozi mkongwe Etienne Tshisekedi aliyeaga dunia Februari.
Baada ya uteuzi huu waziri mkuu atakabiliwa na hali ngumu ya changamoto zinazohusu masuala ya usalama na uchumi. Fedha ya Kongo (Franc) imepoteza karibuni nusu ya thamani yake mwaka jana na uvunjifu wa amani unaotokana na wapiganaji umezidi kuwa mbaya nchini baada ya Kabila kuamua kubakia kwenye madaraka.