Kabila ameonesha matumaini ya kugombea urais DRC 2023

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, Joseph Kabila

Katika mahojiano ya nadra alisema kwa nini tusisubiri mpaka 2013 tuone mambo yatakavyokuwa. Katika maisha kama ilivyo siasa huwezi kufuta uwezekano wowote

Rais Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo-DRC anapanga kubakia katika siasa wakati atakapoachia madaraka baada ya uchaguzi wa Disemba 23 na hafuti uwezekano kwa kuwania tena urais katika uchaguzi wa mwaka 2023 ameliambia shirika la habari Reuters siku ya Jumapili.

Uchaguzi huo uliocheleweshwa unaadhimisha makabidhiano ya kwanza ya madaraka kwa njia ya kidemokrasia na kumaliza utawala wa Kabila ambao ulianza mwaka 2001 baada ya kuuawa kwa baba yake.

Kabila mwenye umri wa miaka 47 alitakiwa aachie madaraka mwaka 2016 wakati muhula wake wa uongozi ulipofikia hatima yake kwa mujibu wa katiba. Lakini uchaguzi wa kumpata mrithi wake ulicheleweshwa mara kadhaa na kuchochea maandamano ambapo darzeni ya watu waliuawa.

Mpaka hivi karibuni haikufahamika kama alikuwa na mpango wa kuwania awamu ya tatu ya uongozi. Anastahili kuwania tena urais mwaka 2023 baada ya kupumzika.

Ramazani Shadary, mgombea urais wa PPRD huko DRC

Kabila alimteua Emmanuel Ramazani Shadary kama mgombea wa ushirika wa utawala. Shadary amewekewa vikwazo na Umoja wa Ulaya kwa shutuma za kuhusika kwake katika ukiukaji wa haki za binadamu. Serikali ya Congo inasema vikwazo ambavyo vinajumuisha marufuku ya kusafiri na kuzuia mali, si halali kisheria.

Ukusanyaji maoni umemuonyesha Shadary ambaye hajulikani sana yuko nyuma ya wapinzani maarufu ambao wanawania uongozi na kuongeza mashaka kwamba huenda akaongoza kwa muhula mmoja tu kabla ya Kabila kurejea katika uongozi.

Joseph Kabila, Rais wa DRC.

​“Kwanini tusisubiri mpaka mwaka 2023 tuone mambo yatakavyokuwa,” amesema Kabila huku akitabasamu katika mahojiano ya nadra kwenye makazi ya rais. “Katika maisha kama ilivyo katika siasa, huwezi kufuta uwezekano wowote,” ameongezea Rais Kabila.