Shirika hilo linaloshirikiana na shirika la ndege la Ufaransa KLM, lilianza safari ndani ya nchi mwezi Julai.
Akizungumza kabla ya ndege ya shirika hilo kuondoka uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta kuelekea London, mkuregenzi wa KQ Allan Kilavuka amesma “tulitangaza kwamba tutaanza tena safari za kimataifa kuelekea sehemu 27 lakini tumeongeza hadi 30 kutokana na ongezeko la mahitaji.”
Amesema kwamba shirika hilo linatarajia ukuaji wake kuwa chini ya asili mia 50 mwaka huu lakini kuna matarajio ya safari za ndege kuongezeka kutokana na mahitaji ya usafiri.
“Tunachukulia mwaka 2020 kama mwaka uliopotea. Mahitaji ya usafiri yamekuwa tu asilimia 25 katika baadhi ya miezi, na asilimia 38 katika miezi mingine,” Kilavuka ameliambia shirika la Habari la Reuters.
Janga la virusi vya Corona limeathiri kabisa sekta ya usafiri kimataifa, mashirika ya ndege ya Afrika yakitarajiwa kupata hasara ya dola bilioni 6 mwaka huu.
Mwezi Julai, shirika la Kenya airways lilisema kwamba lilikuwa linapanga kuwafuta kazi baadhi ya wafanyakazi, lakini halikusema idadi yao.
Kilavuka amesema kwamba kufikia sasa, shirika hilo limefuta kazi wafanyakzi 650, hasa marubani, mafundi, wafanyakazi wa ndani ya ndege na wale waliokuwa wameajiriwa hivi karibuni.
“Kile ambacho ningependa kusisitiza ni kwamba sio kwamba tunataka kufuta watu kazi. Hao wafanyakazi hawajafanya kosa lolote. Ni wafanyakazi wazuri sana lakini ni kwa sababu hatuwezi kuwalipa kwa sasa.”
Shirika la ndege la Kenya airways, liliripoti hasara ya dola milioni 120 mwaka 2019 hata kabla ya janga la virusi vya Corona kutokea.
Soko la hisa la Nairobi, lilisitisha uuzaji wa hisa za shirika la Kenya airways mwezi uliopita kwa mda wa miezi 3 kwa sababu ya kuwepo mipango ya serikali kutaka kumiliki shirika hilo.
Mchakato wa serikali kutaifisha shirikal la KQ bado unajadiliwa bungeni.
Imetayarishwa na Kennes Bwire, VOA, Washington DC.