Jumuiya ya kimataifa yasikitishwa na Mongolia kushindwa kumkamata Putin

Wizara ya Mambo ya Nje ya Ukraine, Jumatatu imesema kushindwa kwa Mongolia kumkamata kiongozi wa Kremlin, Vladimir Putin, aliyetolewa hati ya kimataifa ya kukamatwa kwake kumeleta pigo kubwa kwa mfumo wa sheria ya kimataifa ya uhalifu.

Putin aliwasili Mongolia, Jumatatu kwa mazungumzo ambayo yana uwezekano wa kuangazia bomba jipya la gesi linalounganisha Russia na China.

Hati ya kukamatwa ya Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu iliyotolewa mwaka jana dhidi ya Putin inazilazimisha nchi wanachama 124 wa mahakama hiyo, ikiwa ni pamoja na Mongolia, kumkamata rais huyo wa Russia na kumpeleka The Hague kwa ajili ya kesi yake iwapo atakanyaga katika ardhi yao.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Ukraine, Heorhiy Tykhyi amesema kushindwa kwa Mongolia kumkamata Putin ni pigo kubwa kwa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu na mfumo wa sheria za jinai.