Jumapili Marekani yaadhimisha siku ya haki ya wanawake kupiga kura

Agosti 26 ni maadhimisho ya siku ya haki ya wanawake Marekani kupiga kura

Jumapili ya Agosti 26 ni maadhimisho ya 98 ya siku ya haki ya wanawake kwenye kipengele cha 19 cha katiba ya Marekani kinachowapa wanawake haki ya kupiga kura Marekani. Tangu wakati huo wanawake wamekuwa wakijitokeza kwa wingi kwenye kupiga kura kuliko wanaume.

Mwaka 2016 wanawake milioni 73.7 waliripotiwa kupiga kura ikilinganishwa na wanaume milioni 63.8 kulingana na takwimu kutoka Center for American Women in Politics. Lakini bado kuna vizuizi vingi. Wakati ambapo idadi ya wanawake imeongezeka katika vituo vya kupiga kura katika miongo kadhaa iliyopita utafiti unaonesha bado nafasi ya uwakilishi kwa wanawake ni ndogo katika maeneo mengi ikiwemo serikalini, nafasi za teknolojia na utawala duniani.

Takwimu kutoka Inter-Parliament Union-IPU taasisi ya kimataifa ya wabunge inaonesha kwamba kati ya wabunge wanne duniani kote ni mbunge mmoja tu ndio mwanamke. Nchini Marekani wanawake ni asilimia 25.4 ya kiwango cha baraza la wawakilishi na asilimia 20 ya bunge la Marekani kulingana na takwimu ya kitaifa ya Emily’s List.