Marekani imevuka vifo 600,000 kutokana na COVID-19 kulingana na ripoti ya Jumanne ya kitengo kinachofuatilia virusi vya Corona katika chuo kikuu cha John Hopkins cha Marekani.
Idadi hiyo ni kuanzia mwanzo wa janga hili miezi 15 iliyopita. Wakati idadi ya kesi mpya za COVID-19 na vifo vya kila siku nchini Marekani vinapungua katika wiki za karibuni hatua hiyo ni ukumbusho mzito wa idadi ya vifo vilivyotokana na janga hili na ambavyo bado vinatokea.
Rais wa Marekani Joe Biden alikiri Jumatatu hatua ya ufikiaji wa janga hili akisema kuwa wakati kesi mpya na vifo vinapungua sana nchini Marekani bado kuna watu wengi wanapoteza maisha na hivi sasa sio wakati wa kuwaachia walinzi wetu.
Wakati huo huo huko Uingereza Waziri Mkuu wa nchi hiyo Boris Johnson alitangaza Jumatatu kwamba serikali yake itasogeza mbele kwa takribani wiki nne mpango wake wa kufungua shughuli za umma, kutoka Juni 21 hadi Julai 19 mwaka huu ambapo masharti yote yanayohusiana na COVID-19 yataondolewa.