Kwa mujibu wa shirika la habari la AP, washiriki kwenye kiako hicho cha siku mbili wameomba pande zote za kisiasa nchini Libya kuheshimu makubaliano ya kisiasa, yaliyomaliza uhasama mwaka uliopita. Pia wameombwa waitishe uchaguzi wa rais na bunge mwezi Desemba.
Mkutano huo uliwaleta pamoja mawaziri wa mambo ya nje kutoka Misri, Tunisia, Sudan, Chad na Niger, yakiwa mataifa ambayo kwa muda mrefu yamekuwa yakijaribu kumaliza mzozo wa Libya. Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kwa Libya Jan Kubis, katibu mkuu wa umoja wa mataifa ya kiarabu , ARAB LEAGUE, Ahmed Aboul Gheit ,pamoja na mwakilishi AU pia walihudhuria.
Waziri wa mambo ya nje wa Algeria Ramtane Lamamra wakati akizungumza na wanahabari baada ya kikao hicho amesema kwamba taifa lake ambalo linapakana na Libya liko tayari kusaidia kwa namna yoyote ile.
Tangu mwaka wa 2011, Libya imekumbwa na machafuko baada ya muungano wa NATO kumuondoa madarakani kiongozi wa muda mrefu Moammar Gadhafi, wakati taifa hilo likigawanyika mara mbili kati ya serikali inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa, yenye makao yake makuu mjini Tripoli, na ile inayoongozwa na Khalifa Haftar upande wa mashariki.