Jeshi la Ukraine kujiondoa Avdiivka

Jeshi la Ukraine limesema linajiondoa katika mji wa kusini mashariki wa Avdiivka, wakati huu kukiwa na mzozo wa Russia, na kuongeza kuwa uamuzi huo hautoi fursa za kimkakati kwa Russia.

Kamanda mkuu wa Ukraine, Oleksandr Syrskyi, aliandika kwenye mtandao wa Facebook, kwamba wanajeshi walihamishwa kuepuka kuzingirwa na kuweka usalama kwa maisha na afya ya wanajeshi.

Kamanda wa Ukraine, wa ukanda wa kusini mashariki Oleksandr Tarnavskyi, amesema kupitia mtandao wa Telegram kwamba katika hali ngumu ya uwanja wa mapambano, wajibu wao mkubwa ni kuokoa maisha ya wanajeshi.

Ameongeza kusema kujitoa huko kwa vikosi vya Ukraine kuna athari ndogo. Tarnavskyi alielezea ukanda wa Avdiivka, kama sehemu muhimu kwenye mstari mzima wa mbele wa mapambano, ambao una urefu wa kilomita 1,000.