Jeshi la Somalia lakomboa wilaya muhimu kutoka mikononi mwa al-Shabab

Wanajeshi wa AU wakisha doria nje ya mji wa Burubow uliyopo eneo la Gedi kwenye picha ya maktaba.

Maafisa wa serikali ya Somalia pamoja na wale wa Umoja wa Afrika AU, wamesema Jumanne kwamba jeshi la serikali pamoja na vikosi vya washirika wamewafurusha wapiganaji wa al Shabab kutoka kwenye mji muhimu  katikati mwa taifa, ambapo kundi hilo lilikuwa limelikamata kwa miaka 6.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, jeshi la serikali likisaidiwa na vikosi vya AU limesema kwamba limeua takriban wapiganaji 700 wa al Shabab, huku likikomboa maeneo kwenye operesheni ambayo imekuwepo kwa miezi kadhaa sasa.

Kundi hilo linalohusishwa na al Qaeda limeshika udhibiti wa maeneo kadhaa nchini humo. Mahamud Hasan Mahamud ambaye ni meya wa mji wa Adan Yabal uliopo kwenye jimbo la Middle Shabelle amesema kwamba jeshi lilichukua udhibiti wake pamoja na maeneo jirani, bila makabiliano yoyote mwanzoni mwa wiki.

Wilaya yenye jina sawa na la mji huo ya Adan Yabal ambao sasa imekombolewa ilikuwa muhimu sana kwa al Shabab kwa kuwa unaunganisha kati na kusini mwa Somalia.