Jeshi la Marekani lashambulia vifaa vya Wahouthi nchini Yemen

  • VOA News

Picha iliyotolewa na Kamandi kuu ya jeshi la Marekani Februari 3, 2024 inaonyesha jeshi la Marekani na majeshi shirika wakishambulia ngome za Wahouthi nchini Yemen.

Jeshi la Marekani lilisema Jumapili kwamba lilishambulia vyombo na makombora zaidi katika maeneo yanayodhibitiwa na Wahouthi nchini Yemen ambayo yalikuwa yakiandaliwa kurushwa dhidi ya meli katika Bahari ya Sham.

Mashambulizi hayo yalifanyika Jumamosi kaskazini mwa mji wa Hodeida, kamandi kuu ya Marekani ilisema kwenye mtandao wa kijamii.

Jeshi la Marekani “lilitekeleza kwa mafanikio mashambulizi ya kujihami dhidi ya meli mbili na makombora matatu ya kushambulia meli ambayo yalikuwa yaliandaliwa kurushwa dhidi ya meli katika Bahari ya Sham,” taarifa ya jeshi ilisema.

Kituo cha televisheni cha Wahouthi, Al-Masirah Jumamosi usiku kiliripoti mashambulizi matatu kwenye eneo la bandari ya Salif.

Mashambulizi hayo ni sehemu ya hatua zilizochukuliwa na Marekani na washirika wake dhidi ya Wahouthi, zenye lengo la kuzima mashambulizi ya Mara kwa mara ya waasi hao wanaoungwa mkono na Iran kwenye njia muhimu za meli katika bahari ya Sham.

Jumamosi, Wahouthi walithibitisha kwamba wapiganaji wao 17 waliuawa katika mashambulizi ya hivi karibuni, kufuatia taarifa ya awali ya Marekani siku ya Alhamisi kwamba ilishambulia vyombo vya kurusha makombora.