Jeshi la Kenya ladai kumuua kiongozi wa Al-Shabab

Wanajeshi wa Kenya, katika harakati za kupambana na kundi la Al-Shabab

Jeshi la Kenya linasema limemuuwa mkuu wa ujasusi wa kundi la wanamgambo wa al-Shabaab lenye makao yake Somalia.

Pamoja na taarifa hizo za jeshi le Kenya, kundi la Al-Shabab limekanusha madai hayo.

Msemaji wa jeshi la Kenya, David Obonyo amewaambia wanahabari leo hii kwamba Mahad Karate, ambaye pia anajulikana kama Abdirahim Mohamed Warsame aliuwawa.

Kwa mujibu wa Obonyo, kiongozi huyo aliuwawa pamoja na wanachama wa daraja la kati wengine 10 wa kundi hilo katika shambulizi la anga huko kusini mwa Somalia, Februari 8.

Tovuti inayounga mkono kundi la Al-Shabaab inaripoti kwamba ripoti hiyo ni ya uongo, na kwamba Karate yupo salama.

Inasema hakuna shambulizi lolote la anga lililopigwa kwenye kambi yao.

Wizara ya mambo ya nje ya Marekani imetoa tuzo ya dola milioni tano, kwa taarifa zitakazowezesha kupatikana karate ili afikishwe kwenye vyombo vya sharia.

Inasema anajukumu kubwa katika kundi hilo, la Al-Shabaab ambalo linahusika kwa mashambulizi kwenye chuo kikuu cha Garissa, Kenya yaliyofanyika April mwaka jana na kuuwa takribani watu 150.