Jeshi la Israel limeomba radhi Jumatatu kwa kuwauwa wanajeshi watatu wa Lebanon katika shambulizi kusini mwa Lebanon, wakati mjumbe wa Marekani alipowasili mjini Beirut kwa mazungumzo na maafisa wa Lebanon kuhusu uwezekano wa masharti ya kusitisha mapigano kati ya Israel na kundi la wanamgambo la Hezbollah lenye makao yake nchini Lebanon.
Msemaji wa jeshi la Israel amesema shambulizi la Jumapili lilipiga gari linalomilikiwa na jeshi la Lebanon na kwamba Israel haifanyi operesheni dhidi ya jeshi la Lebanon.
Ziara ya mjumbe wa Marekani, Amos Hochstein mjini Beirut ilijumuisha mazungumzo yaliyopangwa na Najib Mikati, waziri mkuu wa muda wa Lebanon, pamoja na Nabih Berri, spika wa bunge.
Katika kuongezea juhudi za kusitisha mapigano kati ya Israel na Hezbollah, Marekani pia inawashinikiza wabunge wa Lebanon kusonga mbele kumchagua rais kama sehemu ya msukumo wa kuimarisha taasisi za serikali.