Jeshi la Israel limeingia Lebanon

Moshi kutokana na mabomu ya Israel karibu na mpaka wa Israel na Lebanon Oct. 8, 2024

Jeshi la Israel limetangaza kwamba limeanzisha oparesheni za ardhini kusini magharibi mwa Lebanon, ikiwa ni hatua ya kupanua uvamizi wake ambao maafisa wa Israel wamesema unalenga kuwasukuma nyuma wanamgambo wa Hezbollah kutoka mpakani.

Jeshi la Israel limetaja juhudi zake mpya ni za kimkakati na katika sehemu maalum.

Operesheni hiyo ya ardhini pia inahusisha mashambulizi ya anga, ikiwemo mashambulizi mapya ya anga ya Jumanne, katika eneo la Dahieh, mjini Beirut.

Jeshi la Israel limesema kwamba shambulizi la anga lilimuua kamanda wa ngazi ya juu wa Hezbollah Suhail Hussein, ambaye alihusika kusafirisha silaha kutoka Iran kupeleka kwa wanamgambo wa Hezbollah, nchini Lebanon.

Shambulizi hilo lilijiri siku 10 baada ya shambulizi jingine la Israel kumuua kiongozi wa Hezbollah Hassan Nasrallah, wakati Israel inaongeza kampeni yake la kijeshi nchini Lebanon.

Naibu kamanda wa Hezbollah Naim Qassema amesema kwamba kundi hilo lipo thabithi na limekabiliana na mapigo machungu ambayo lililopata hivi karibuni.