Jeshi la Israel limesema Alhamisi kuwa lilifanya mashambulizi ya anga ambayo yaliwaua makamanda wawili wa Hezbollah ambao walihusika katika mashambulizi ya makombora yaliyolenga eneo la kaskazini mwa Israel. Jeshi la Ulinzi la Israel liliwataja makamanda hao kuwa ni Ahmad Moustafa al-Haj Ali na Mohammad Ali Hamdan.
Jeshi la Israel pia limesema Alhamisi kwamba limegundua makombora mapya 40 ambayo yalirushwa kutoka Lebanon na kuingia katika eneo la Israel, ambayo baadhi yake yalitunguliwa na ulinzi wa anga wa Israel.
Rais wa Marekani Joe Biden amezungumza na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu siku ya Jumatano, akisisitiza msaada wake wa kuiunga mkono Israel wakati ikiendelea na operesheni zake za kijeshi dhidi ya wanamgambo huko Gaza na Lebanon na anafikiria jibu kwa mashambulizi ya karibuni ya makombora ya Iran.