Jeshi la DRC linasema limeua waasi 11 wa ADF

Magari ya wanajeshi wa DRC yakisindikiza magari ya raia yanayosafirisha bidhaa kutoka mji wa Beni kuelekea mji wa Komanda, Machi 19, 2022. Picha ya AFP

Jeshi la DRC Jumanne limesema limewaua waasi 11 wa kundi la wanamgambo la Allied Democratic Forces (ADF), ambalo kundi la kigaidi la Islamic State linadai ni mshirika wake, mashariki mwa DRC.

ADF ni mmoja ya makundi yanayofanya ukatili mkubwa kati ya zaidi ya makundi 120 yaliyopo katika eneo la mashariki mwa DRC lenye mzozo.

Kundi hilo limelaumiwa kwa maelfu ya vifo katika mikoa ya Kivu Kaskazini na Ituri, na kwa mashambulizi ya mabomu mwaka jana nchini Uganda.

Msemaji wa jeshi la Congo katika mji wa Beni katika jimbo la Kivu Kaskazini, Kepteni Antony Mualushayi, amesema wanajeshi waliwaua wapiganaji 11 wa ADF jana Jumanne.

Siku moja kabla, wanajeshi waliwaua wapiganaji wanane wa kundi la Mai Mai Mazembe katika wilaya ya Lubero huko Kivu Kaskazini. Mualushayi ameongeza kuwa, wanajeshi wawili waliuawa wakati wa mapigano hayo.

Rais wa DRC Felix Thisekedi alibadilisha viongozi wa kiraia wa Kivu Kaskazini na Ituri na kuwaweka maafisa wa kijeshi katika harakati za kumaliza ghasia.

Hata hivyo, mashambulizi ya waasi dhidi ya raia yaliendelea.