Jeneza la mabaki ya Lumumba lawasili DRC kwa ajili ya mazishi

Waziri mkuu wa DRC Sama Lukonde akisimama karibu na jeneza la shujaa wa uhuru wa Congo Patrice Lumumba wakati wa hafla ya kutoa heshima, kwenye ubalozi wa DRC mjini Brussels kabla ya mabaki yake kurejeshwa Congo, June 21, 2022. Picha ya AFP

Jeneza la shujaa wa uhuru wa Congo aliyeuawa Patrice Lumumba limerejeshwa nchini mwake Jumatano kwa ajili ya mazishi, zaidi ya miongo sita baada ya kuuawa kwake.

Ndege ilichukua mabaki ya Lumumba, hasa jino ambalo Ubelgiji, mkoloni wa zamani wa Congo, ilikabidhi kwa familia yake Jumatatu, kutoka Brussels hadi Kinshasa, mabaki hayo yatasifirishwa kote nchini DRC kwa siku tisa.

Jeneza na wajumbe walioandamana nalo walisafiri kwa ndege hadi mkoa wa kati wa Sankuru, ambako kiongozi huyo wa kwanza wa nchi hiyo baada ya uhuru alizaliwa katika kijiji cha Onalua mwaka wa 1925.

“Mheshimiwa waziri mkuu wangu wa kwanza, polisi na wanajeshi wa DRC wamejipanga kukupa heshima zao ukirejea kijijini mwako,” afisa wa polisi aliyesimama kwa umakini amesema, mbele ya jeneza lilipowasili kwenye uwanja wa ndege katika mji wa Tshumbe.

Kutoka hapo, lilipelekwa kilomita 25 hadi Onalua, ambako siku mbili za kutoa heshima zimepangwa.

Mabaki hayo yatapelekwa kwenye maeneo muhimu kwa maisha ya Lumumba na kuzikwa katika kaburi mjini Kinshasa tarehe 30 mwezi huu, kufuatia siku tatu za maombolezo ya kitaifa.