Jenerali wa jeshi la Syria auawa

Majeshi ya Syria yaripotiwa kuendelea na mashambulizi yake dhidi ya upinzani na kusababisha uharibifu mkubwa wa mali na watu.

Watu wenye silaha wamuua Brigadia-jenerali wa jeshi la Syria.

Shirika la habari linalomilikiwa na serikali nchini Syria linasema watu wenye silaha wamempiga risasi na kumuua afisa wa juu wa jeshi la nchi hiyo katika mji mkuu, Damascus.

Shirika la habari la SANA linasema watu watatu waliokuwa na bunduki walimfyatulia risasi Brigadia-jenerali Issa al-Khouli Jumamosi asubuhi wakati akiondoka nyumbani kwake katika eneo la Rukn-Eddin.

Mapigano pia yameripotiwa kwa usiku mzima katika mji mkuu kati ya waasi wa Free Syrian Army na wanajeshi wa serikali.

Mivutano bado iko juu kote nchini humo wakati majeshi ya usalama yakizidisha ukandamizaji wake kwenye maeneo ya upinzani.

Picha za karibuni za satalaiti kutoka katika Digital Globe yenye makao yake nchini Marekani zinasemekana kuonyesha vifaru vya jeshi la Syria na magari mengine ya kivita yakiwa karibu na maeneo ya wapinzani katika mji wa Homs ambao ni kiini cha upinzani. Makundi ya haki yanasema zaidi ya watu 300 wameuawa katika muda wa wiki moja iliyopita ikiwa ni sehemu ya ukandamizaji wa serikali kwenye maeneo ya waasi.