Mjumbe maalum wa Marekani kwa pembe ya Afrika, Jeffery Feltman, aliwasili mjini Khartoum leo Jumanne kujaribu kupunguza mzozo kufuatia mapinduzi ya wiki iliyopita, yaliyofanywa na jenerali wa juu wa Sudan, kituo cha televisheni cha al-Arabiya chenye makao yake Dubai kiliripoti.
Jenerali Abdel Fattah al-Burhan alilifuta baraza la mawaziri la Waziri Mkuu, Abdalla Hamdok hapo Oktoba 25 na kumuweka katika kifungo cha nyumbani na kusababisha mataifa ya magharibi kukata misaada ya mamilioni ya dola kwa Sudan. Waziri wa mambo ya nje wa Marekani, Antony Blinken, siku ya Alhamis alilaani jeshi kukamata madaraka, na kukamatwa kwa viongozi wa kiraia wa Sudan.
Mapinduzi hayo ymaevuruga kipindi cha mpito kilichokuwa kinaielekeza Sudan kwenye demokrasia na uchaguzi mkuu mwaka 2023, baada ya mtawala wa muda mrefu, Omar al-Bashir kuondolewa madarakani mwaka 2019.