Jammeh wa Gambia aachia madaraka

Yahya Jammeh akiwaaga wafuasi wake

Rais aliyeshindwa uchaguzi Yahya Jammeh ameondoka nchini Gambia Jumamosi Usiku na kwenda nchini Equatorial Guinea.

Hatua hiyo imehitimisha utawala wake wa miaka 22 wa kidikteta na migogoro ya kisiasa ambayo ilipelekea nchi hiyo ya Afrika Magharibi kufikia katika hali ya majeshi ya kieneo kuingia kwa nguvu kumuondosha mtawala huyo madarakani.

Jammeh hakutoa tamko lolote wakati anaondoka kwenye uwanja wa ndege wa Banjul na familia yake katika ndege iliyokuwa haina alama yoyote, na kwenda nchini Equatorial Guinea.

Alikuwa amefuatana na Rais wa Guinea, Alpha Conde, ambaye alipendekeza awe msimamizi wa kutafuta ufumbuzi juu ya njia ya kumuondosha nchini kwa kuzungumza naye.

Kuondoka kwake Jammeh, ambaye alichukuwa madaraka kwa njia ya mapinduzi mwaka 1994, kumemaliza wiki kadhaa za mvutano zilizoanza mara alipokataa kuachia madaraka kufuatia ushindi aliopata mpinzani wake katika uchaguzi wa mwezi Desemba 1.

Pia kuondoka kwake kumeepusha uingiliaji kati wa jeshi lenye askari 7000 kutoka Senegal na Nigeria ambao tayari walikuwepo nchini Gambia Alhamisi ili kukabiliana na wafuasi wa Jammeh katika jeshi lake.

Kwa pamoja Umoja wa Afrika na baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa walikubaliana mpango wa kutumia majeshi kumtoa madarakani Jammeh.

Kuondoka kwake kumefungua njia kwa Adama Barrow kuchukua madaraka, ambaye alishinda uchaguzi wiki saba zilizopita.

Barrow ambaye aliapishwa Alhamisi kwenye ubalozi wa Gambia nchini Senegal, hivi sasa anatarajiwa kurejea nyumbani.

Rais mpya wa Gambia Adama Barrow

Mapema wiki hii, Jammeh alitangaza hali ya hatari katika juhudi zake za mwisho za kubakia madarakani.

Alilivunja baraza lake la mawaziri wakati bunge la nchi hiyo likamuongezea muda wa miezi mitatu madarakani.

Lakini Ijumaa shinikizo lilikuwa kubwa na aliendelea kufanya mazungumzo na marais wa Guinea na Mauritania kabla hajakubali kuachia madaraka.

Vyanzo vya habari vimesema kuwa mazungumzo hayo yalijiri juu ya sehemu gani angekwenda Jammeh kuishi na iwapo atapewa msamaha kwa makosa ya jinai aliyotenda wakati wa utawala wake.

Barrow, ambaye ni mfanyabiashara wa ujenzi wa majumba, alisheherekea wakati ilipokuwa bayana Ijumaa kwamba Jammeh hana hila tena ni lazima aondoke.

“Utawala wa vitisho umezimwa kabisa sasa nchini Gambia,” Barrow amesema akiwa Dakar wakati akijiandaa kurundi nyumbani Gambia.