Jamii ya Kimataifa Yamshtumu Ghadafi.

  • Dina Chahali

Waandamanaji wanaopinga kiongozi wa Libya wabeba mabango ya picha zake wakimtaka ajiuzulu mjini Brussels, Ubelgiji Februari 25, 2011

Ghasia na maandamano yameendelea Libya Ijumaa huku jamii ya kimataifa ikitafakari juu ya kuchukua hatua dhidi ya dikteta Moammar Ghadafi.

Msukumo wa kimataifa unaongezeka dhidi ya kiongozi wa Libya Moammar Gadhafi ambaye msako wake mkali dhidi ya upinzani umeleta shutuma kali kutoka maeneo mbali mbali.

Mkuu wa sera za nje waUmoja wa Ulaya Catherine Ashton alisema Ijumma kuwa jumuiya hiyo ya mataifa 27 lazima ifikirie kuchukua hatua kali dhidi ya Libya ikiwa ni pamoja na kudhibiti mali zake.

Wakati huo huo vuguvugu la kupinga serikali kadhaa katika nchi za kiarabu linaendelea kushika kasi huku maandamano mengi yakifanywa na umati mkubwa wa watu baada ya Swala ya Ijumaa katika kile walichokiita ‘Siku ya Hasira”. Maandamano hayo yaliripotiwa nchini Iraq , Misri, Yemen na kwingineko.

Huko nchini Tanzania, waziri wa Mambo ya nje ya ushirikiano wa kimataifa Bw. Bernard Membe aliwaonya raia wa Tanzania walioko nchini Libya dhidi ya kujiingiza katika vurugu za kisiasa zinazoendelea nchini humo.