Akizungumza na idhaa ya Kiswahili VOA Jumatatu mwanzilishi mwenza wa mtandao wa Jamii Forums, Mike Mushi aliyeko Arusha, Tanzania, amesema kanuni hiyo mpya ina vipengere ambavyo ni shida kuvitimiza.
“Ikiwa tutakubali kufanya hivyo ina maana tutakuwa tunaingilia faragha ya watumiaji wetu. Kanuni pia inalazimisha kufanya kazi na vyombo vya ulinzi na usalama. Lakini kanuni inalazimisha kuwa taarifa za watu lazima tuzitume kwa kipindi cha miezi 12,” ameeleza.
Kifungu cha 5,e, cha kanuni ya sheria mpya ya mtandaoni kinasema ni lazima uweke njia za kupata taarifa binafsi za wachangiaji wanaoweka maudhui kwenye mtandao husika.
Kwa upande wa mitandao ya kimataifa Kanuni imewaondolea kizuizi, wao hawaguswi na kanuni hii, lakini Watanzania wote ni lazima wachukue leseni.
Bado tunatafuta njia ya kukaa na TCRA na kuwaelewesha, kwa kuongea nao na kufikisha ujumbe wetu na kuelezea kitu hiki kitakuwa kigumu kwa upande wetu.
“Ni matumaini yetu mazungumzo haya yatazalisha matunda chanya ili jamii forums iweze kurudi hewani.