Baraza la seneti la Jamhuri ya Congo siku ya jumatatu lilipiga kura ili kufanya marekebisho ya baadhi ya utaratibu wa ulipaji madeni yake kwa China hatua ambayo shirika la kimataifa la fedha-IMF lilisema ilikuwa muhimu ili kuwezesha msaada wa kifedha kutolewa kwa nchi hiyo.
Mashauriano juu ya kutolewa msaada wa kifedha kuokowa uchumi wa taifa hilo linalotegemea mafuta yalikuwa yanadorora tangu mwaka 2017 wakati maafisa wa Congo waliposhindwa kuishawishi IMF kwamba walikuwa wakifanya vya kutosha kudhibiti deni la kitaifa au kukabiliana na rushwa.
Kutokana na juhudi hizo ujumbe wa IMF ulieleza mwezi huu wa Mei kwamba ulikubaliana na serikali ya Congo juu ya mpango wa miaka mitatu wa kutoka mkopo ikiwa mageuzi yatatekelezwa na kuidhinishwa na bodi ya wakurugenzi wa IMF.