Dk. Willy Mtunga aliyeteuliwa kuchukua kiti cha jaji mkuu wa Kenya alifanya kitu ambacho hakuna jaji yeyote wa Kenya aliyewahi kufanya: alitetea hadharani uteuzi wake katika wadhifa huo.
Kufuatana na katiba mpya ya Kenya maafisa wa vyeo vya juu wanapoteuliwa wanabidi kuidhinishwa na bunge laKenya kabla ya rais kutangaza uteuzi wao.
Katika kikao cha kwanza Jumanne, cha kamati ya masuala ya sheria na katiba ya bunge kilichongozwa na Abdikadir Mohammed na kurushwa moja kwa moja kwenye televisheni, wajumbe walimuandama Mutunga kwa maswali kuhusu rikodi yake na kutaka kujua amejiandaaje kuongoza mfumo wa sheria Kenya unaokabiliwa na shutuma nyingi hasa ulaji rushwa.
Kiongozi wakamati hiyo alisema Kenya inahitaji mtu ambae ataweza kufanya mageuzi muhimu ndani ya mahakama na alimuuliza Mutunga ataihakiishia vipi tume hiyo juu ya uteuzi wake kama kiongozi katika chombo hicho cha dola kinachohitaji mageuzi mengi kufanyika.
Haruni Ndumbi, wakili na mwenyekiti wa taasisi ya Shelter Forum, akizungumza na Sauti ya Amerika anasema wakenya inabidi wajivuniye hivi sasa kuona kwamba katiba waloidhinisha imeanza kufanyakazi na ni matumaini yake itawalazimisha viongozi wapya kuwajibika mbele ya wananchi.