Malumbano ya hadharani yalindelea kushuhudiwa kati ya jaji huyo mkuu na wanasiasa wa mirengo yote miliwili, licha ya Maraga kuwahakikishia Wakenya kwamba mahakama ziko tayari kusikiliza na kutatua mizozo yoyote itakayoibuka kufuatia uchaguzi wa Jumanne.
Haya yalijiri wakati jaji huyo anaendelea kukabiliwa na shinikizo kutoka kwa wanasiasa, baadhi yao wakitaka majaji fulani kutosikiliza kesi hizo, iwapo zitawasilishwa mahakamani.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Nairobi, Maraga alisema kwamba licha ya shutuma zinazotoka kwa baadhi ya Wakenya, mahakama hizo zitafanya kazi usiku na mchana, na hata wikendi, ili kuzisikiliza kesi za uchaguzi katika muda uliowekwa kikatiba.
"Kwa mujibu wa sheria, kesi hizi ni lazima zisikilizwe katika kipindi cha siku 14," alisema jaji Maraga.
Aidha Maraga alizindua kitabu cha kanuni wanazotakiwa kufuata majaji wakati wa kuamua kesi zinazohusu uchaguzi.
Haya yalijiri wakati ambapo idara ya mahakama imeendelea kupata shinikizo kutoka kwa wadau mbali mbali, huku wengine wakiwataka baadhi ya majaji kujiondoa kutoka kwa kesi ambazo huenda zitawasilishwa baada ya uchaguzi na kusema kuwa wengine wana mnasaba na baadhi ya viongozi.
Siku ya Jumatano, jaji Maraga aliwataka wanasiasa kutoingilia masuala ya utenda kazi wa mahakama na kuwataja viongozi wa kisiasa, wakiwemo rais Uhuru Kenyatta, kiongozi wa chama cha ODM na mgombea wa urais wa muungano wa NASA, Raila Odinga, pamoja na kiongozi wa walio wengi katika bunge, Aden Duale, kama baadhi ya watu wanaoingilia shughuli za mahakama kwa njia isiyofaa.
Pande zote mbili zimeelezea kutoridhika kwake na baadhi ya maamuzi ya mahakama, hususan wakati kesi hazikuamriwa kama walivyopenda.
Na baada ya jaji mkuu kumsuta kiongozi wa wengi bungeni, siku ya Alhamisi, mbunge wa Garissa mjini Aden Duale, ameendelea kulalamika kwamba chama cha Jubilee hakina Imani na jaji wa mahakama kuu, George Odunga.
Akizungumza na kituo cha televisheni cha KTN akiwa mjini Garisa, Duale alitaka jaji mkuu kumshinikisha jaji Odunga kujiondoa kwa kesi zinazohusu uchaguzi kwani, kilingana na Duale, ana uhusiano wa karibu na viongozi wa muungano wa NASA.
Lakini jaji mkuu wa Kenya ameshikilia kwamba hana mamlaka ya kumtaka jaji mwingine kujiondoa kutoka kwa kesi yoyote.
Haya yanajiri huku wagombea wakuu wa urais Uhuru Kenyatta, na Raila Odinga,wakikita kambi katika maeneo mbalimbali kuwarai wapiga kura kuwapa nafasi ya kuwahudumia kutoka ikulu.
Odinga na ujumbe wakla walikuwa katika Magharibi ya Kenya, huku Kenyatta na wenzake wakifanya kampeni katika kaunti za Meru, Tharaka Nithi na Kitui.
Imeandikwa na BMJ Muriithi akiwa Nairobi, Kenya.