Italia yajitoa kwenye mpango wa BRI wa China

Italia imeifahamisha rasmi China, kujitoa kwenye mpango wa miundombinu wa BRI, na kuwa nchi ya kwanza kufanya hivyo tangu mpango huo kuzinduliwa muongo mmoja uliopita.

Licha ya uamuzi huo, Roma inapanga kudumisha uhusiano mzuri na Beijing, vyanzo vya serikali vimesema Jumatano.

Beijing ilizindua BRI, mpango wa kimataifa wa miundombinu na usafiri, 2013, ukilenga kuimarisha uhusiano wa China na mataifa ya Ulaya na Asia, Afrika, Pacific na Amerika Kusini.

Wakosoaji wanasema lengo moja kuu ni kupanua ushawishi wa chama cha kikomunisti cha China.

Karibu nchi 150, ambazo ni karibu asilimia 75 ya idadi ya watu ulimwenguni, wamejiunga.

Waziri mkuu wa Italia, Giorgia Meloni, kwa muda mrefu amekuwa akikosoa ushirikiano huo, wakati fulani aliuita uamuzi wa 2019 wa kujiunga na BRI kuwa kosa kubwa.

Baada ya Meloni kuchukua madaraka mwaka jana, alisema ahadi za kiuchumi za mpango huo hazijawahi kutimizwa.