Jeshi la Israel, limetoa amri ya kuondoka katika mji wa Gaza, Jumatano, ikiwaeleza Wapalestina kuelekea maeneo ya kati na kusini ambayo yameshuhudiwa na vifo katika kipindi cha saa 48 zilizopita.
Amri ya kuondoka ilitolewa kupitia vipeperushi vilivyo rushwa kutokea angani vikieleza eneo hilo litaendelea kuwa hatari la mapambano.
Vipeperushi hivyo vilionyesha njia mbili salama ambazo watu wanapaswa kuzitumia kuondoka katika mji huo.
Amri hiyo imetolewa wakati vikosi vya jeshi la Israel, vikiendelea na mashambulizi yao katikati mwa Gaza, Jumatano, siku moja baada ya shambulizi la anga kupiga shule ambayo iligeuzwa makazi ya Wapalestina waliokimbia makazi yao na kuuwa takriban watu 29 kwa mujibu wa maafisa wa afya wa Palestina.
Jeshi la Israel lilifanya mashambulizi katika miji ya Nuseirat na Khan Younis, na kuuwa watu sita na kujeruhi kadhaa kwa mujibu wa taarifa za vyombo mbalimbali vya habari.