Serikali ya Israel, Jumapili ilitangaza rasmi kuwa vitani dhidi ya wanamgambo wa Hamas huko Gaza, na kuweka mazingira ya jeshi la Israel kujibu shambulizi la kushtukiza la kundi la wanamgambo wa Hamas dhidi ya taifa hilo la Kiyahudi.
Waziri mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, tayari Jumamosi alisema nchi yake ipo vitani na Hamas huku mashambulizi ya wanamgambo hao yakiendelea, lakini kauli yake hiyo hikuwa rasmi.
Uamuzi ulio fanywa na baraza la mawaziri Jumapili umefanya tamko hilo la vita kuwa rasmi.
Kabla ya kura ya baraza la mawaziri, Netanyahu, alitangaza kwamba Israeli italipiza kisasi kikubwa dhidi ya Hamas, licha ya wanajeshi wa Israeli tayari walipoanza kupambana na wapiganaji wa Hamas, Jumapili katika mitaa ya kusini mwa Israeli na kuanzisha mashambulizi ya anga ya kulipiza kisasi ambayo yaliharibu majengo ya Gaza.